NEWS

29 Septemba 2019

VIDEO: ALICHOHUTUBIA PROF KABUDI, UMOJA WA MATAIFA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi akihutubia Mkutano wa 74 wa Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi amehutubia Mkutano wa 74 wa Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani mbele ya viongozi wa dunia na katika hotuba yake hiyo Ijumaa usiku, Septemba 27, 2019 ametilia mkazo mambo matatu ambayo Serikali ya Tanzania inayasimamia.

 

Miongoni mwa masuala hayo ni pamoja na Tanzania kujidhatiti katika kupambana na janga la tabia nchi ambapo alisema tayari Tanzania imepiga hatua kubwa na kutolea mfano wa kuhifadhi misitu yake na kujenga bwawa kubwa la umeme litakaloifanya bei ya umeme iwe nafuu kwa Watanzania wote na hivyo kudhibiti ukataji miti hovyo inayotumika kama nishati mbadala na wananchi wengi wa kipato cha chini.

 

“Kwa hiyo tunaungana kabisa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika kuhakikisha kwamba nchi zetu zinazoendelea zinasaidiwa kupata maendeleo na wakati huo huo kuhifadhi mazingira. Na maana yake wote tuna wajibu wa pamoja wa kulinda mazingira, lakini kila mtu ana wajibu ulio tofauti.

“Wao waliochafua mazingira lakini sasa wana mali za kutosha, wana wajibu wa kutoa fedha, teknolojia ya kupambana na hiyo hali na sisi tuna wajibu wa kushiriki katika miradi hiyo ili kunusuru na kuikoa dunia isiangamie mapema kuliko inavyotarajiwa.” Alisema Profesa Kabudi.

 

Aidha Prof Kabudi, alitumia nafasi hiyo kuziomba jumuia za kimataifa kuliangalia kwa kina suala la Zimbabwe dhidi ya vikwazo ambavyo vimesababisha hali ya maisha ya wananchi wengi kuwa ngumu zaidi.

 

Waziri Kabudi pia ameieleza Jumuia ya Kimataifa kuwa ni wakati sasa wa Afrika kuwa Bara litakalojiletea maendeleo ya viwanda na kuachana na kasumba ya kuuza malighafi kwenye masoko ya Ulaya badala yake waanze kujenga viwanda ili kuimarisha uchumi na kuwapatia ajira vijana.

 

Kuhusu kile ambacho Tanzania inataka kuona kwenye maeneo ya ulinzi wa amani hususan kule Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambako imepeleka askari kwenye kikosi maalum, Waziri Kabudi ambaye ndiye kiongozi wa ujumbe wa Tanzania kwenye UNGA 74, amesema, “Tanzania ingependa muhula wa majeshi ya ulinzi wa amani ya MONUSCO uongezwe lakini ile brigedi ambayo Tanzania inashiriki ya kuhakikisha inapambana na magaidi na vikundi vyenye silaha ambayo vinaua watu kule DRC vidhibitiwe.”

 

Ili kufanya hivyo Prof Kabudi amesema, umefika wakati kwa Umoja wa Mataifa kuiwezesha hiyo bridgedi maalum kwa kuwa na uwezo wa silaha au nyenzo za kisasa ili iweze kupambana na vikundi hivyo vya kujihami .

The post VIDEO: ALICHOHUTUBIA PROF KABUDI, UMOJA WA MATAIFA appeared first on Global Publishers.