NEWS

1 Oktoba 2019

Kofia nyekundu za Peoples power zapigwa marufuku Uganda

Wanasiasa wa upinzani nchini Uganda chini ya vugu vugu la Peoples Power linaloongozwa na mbunge msaanii Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine, wataendelea kuvaa mavazi ya vugu vugu lao, licha ya jeshi la UPDF kutangaza mavazi yao mapya ikiwa na kofia inafanana na ya Peopes Power.

Msanii na mwanasiasa wa upinzani Bobi Wine, amekua akivalia kofia nyekundu kama ''nembo ya uasi''.

Japo Bobi Wine hajatoa tamko lolote kuhusiana na sheria hiyo mpya lakini baadhi ya viongozi wa waandamizi wa vugu vugu la People Power wameliambia shirika la habari la AFP kwamba wataendelea kuvaa kofia hiyo.

"Tutaendelea kuvaa kofia zetu nyekundu," alisema kiongozi wa vijana Ivan Boowe. "Hakuna mtu atakayetutisha wala kututia uoga kwa kupigania haki yetu."

"Kwa kujumuisha kofia yetu katika sare za kijeshi, serikali inapanga njama ya kupiga marufuku vugu vugu la People Power na tuko tayari kukabiliana na hatua itakayotekelezwa na serikali,"aliongeza.

Jeshi la uganda UPDF limefanya mabadiliko katika sare zake za kijeshi katika vikosi mbali mbali na kutangaza katika gazeti rasmi la serikali hapo jana.

Hii ni baada ya kuidhinishwa tarehe 18 mwezi huu wa Septemba na baraza la kijeshi.

Kufuatia sheria za jeshi mtu yoyote atakayevaa sare za jeshi atachuliwa hatua za kisheria na kufunguliwa mashitaka katika mahakama ya kijeshi.