NEWS

27 Novemba 2019

Serikali yatoa Tahadhari kwa Walaji wa Nguruwe


Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, alitoa tahadhari hiyo wakati akifungua mkutano wa kwanza wa kimataifa jana wa kujadili minyoo ya tegu wa nguruwe, jijini hapa.

Dk. Ndugulile, alisema serikali haijapata chanjo ya kumzuia mnyoo huyo wa nguruwe na ipo katika utafiti wakuangalia namna ya kumdhibiti.

Alisema walaji wa nguruwe wafahamu kuwa kuna minyoo inayopatikana kwenye nyama hiyo kupitia mayai na inaweza kumuathiri binadamu endapo atakula nyama isiyopikwa vizuri na mboga ambazo hazijaoshwa na kupikwa vizuri.

Dk. Ndugulile alisema athari zinazotokana na kula nyama hiyo ni kubwa ikiwamo kupata ugonjwa wa kifafa, tatizo ambalo limeshaingia nchini na limeanza kuathiri zaidi mikoa ya Manyara, Njombe, Mbeya, Sogwe na Arusha, huku asilimia 16 ya wananchi wanaoishi mikoa hiyo wakiathirika kwa ugonjwa huo.

"Jinsi ya kutokomeza ugonjwa huu wa minyoo wa tegu wa nguruwe, ni wafugaji kufuga kisasa na kuacha wanyama wao kuzurura ovyo kwa sababu huacha kinyesi chenye mnyoo huyo katika mboga,” alisema.

Pia, aliwataka wafugaji kupata ushauri kitalaamu wa mifugo na wachinjaji wasichinje bila kizingatia utaalamu unaosimamia wanyama hao. Aliwataka wanaokula nyama hiyo kuhakikisha inapikwa vizuri na kuiva.

Hata hivyo, alisema wafugaji wanaweza kuzuia kwa mifugo yao kuzagaa na kupima mnyama kabla ya kuchinja.

Mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya magonjwa ya binadamu (NIMR), Prof. Yunus Mgaya, alisema wanatekeleza mradi huo kwa kukusanya taarifa za mnyoo huyo mbaye anapatikana kwa kula mboga zilizobeba mayai yaliotokana na vinyesi vya nguruwe au kinyesi cha binadamu.

"Mradi huu unatekelezwa na nchi zingine mbili Afrika Msumbiji na Zambia na tunashirikiana na wadau wetu wa utafiti wa Ujerumani kutoka Chuo Kikuu cha Munchen,” alisema.

Kaimu Mkuu wa idara ya tiba ya mifugo na afya ya jamii ambaye pia ni Mkurugenzi wa mtandao wa utafiti wa kisayansi Prof. Helena Ngowi, alisema mnyoo huyo ni hatari kwa sababu anaweza kuleta adhari katika utumbo na ubongo wa binadamu.