NEWS

6 Septemba 2020

Majaliwa Aeleza Hakuna Tatizo la Bima ya Afya Tanzania



Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amewataka wananchi wasikubali kupotoshwa kwa kuwa hapa nchini hakuna tatizo la huduma za Bima ya Afya na kuwasisitiza waendelee kuiamini Serikali yao.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Jijini Arusha na kusema kuwa Serikali imeweka mikakati madhubuti inayowawezesha wananchi kutibiwa, ikiwa ni pamoja na kupitia Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), ambapo wananchi wanachangia kiasi kidogo na Serikali inawaongeza na kuwawezesha kutibiwa bure wao na familia zao.

Waziri Mkuu pia ameutaja utaratibu mwingine ambao ni kupitia Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), ambao ni maalumu kwa ajili ya watumishi wa umma, kuchangia kiasi kidogo kupitia mishahara yao na mpango huo unawawezesha kutibiwa bure, hivyo hakuna tatizo la huduma ya bima ya afya nchini. Amewataka wananchi wasikubali kupotoshwa na waendelee kuiamini Serikali yao.

Aidha Waziri Mkuu ameongeza kuwa katika ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020 hadi 2025, imeilekeza Serikali kuimarisha mfumo wa bima ya afya nchini ikiwamo Mifuko ya Bima za Afya (NHIF na CHF), ili kufikia lengo la Serikali la kuwa na Bima ya Afya kwa wananchi wote.