NEWS

18 Desemba 2020

Waziri Jafo Ahimiza Amani Kwa Maendeleo Ya Nchi

 


Na Ramadhani Kissimba, Dodoma
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mheshimiwa Selemani Jafo amewataka wahitimu wa vyuo vikuu na Watanzania kwa ujumla kuhakikisha wanalinda amani ili nchi iweze kupiga hatua kubwa kiuchumi na kuzishinda hila za watu wasiolitakia mema Taifa walioko ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Mheshimiwa Jafo ametoa rai hiyo mkoani Dodoma wakati akiwatunuku vyeti wahitimu 4,072 wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo vijijini Kampasi Kuu ya Dodoma waliohitimu kozi 26 zinazohusu mipango ya maendeleo, uchumi, idadi ya watu, rasilimali watu, uwekezaji, mazingira na usimamizi wa miradi.

Alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli nchi imepiga hatua kubwa kimaendeleo ikiwemo utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati hatua ambayo maadui wa ndani na nje ya nchi wasioitakia mema nchi wameanza kuleta chokochoko.

Aliitaja baadhi ya miradi hiyo inayoonewa kijicho na watu mbalimbali wasioitakia mema nchi kuwa ni ujenzi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere lenye uwezo wa kuzalisha zaidi ya megawati 2000 za nishati hiyo, ujenzi wa Reli ya Kisasa, ununuzi wa ndege 11 pamoja na ujenzi wa miundombinu ya barabara inayojengwa kila kona nchini.

Aliwataka wahitimu hao kuhakikisha kuwa wanalinda na kudumisha amani ya nchi ili waweze kufanyakazi zao kwa amani na utulivu na kuiwezesha nchi kukua zaidi kiuchumi ambapo amesisitiza kuwa ukuaji wa kasi wa uchumi wa nchi umeiwezesha Tanzania kuingia katika uchumi wa kati kabla ya muda uliopangwa kwenye dira ya Maendeleo ya Taifa mwaka 2025.

Aidha, Mheshimiwa Jafo aliwashauri wahitumu hao kujiunga kwenye vikundi vya maendeleo na kujiajiri wenyewe na kwamba Serikali kupitia Halmashauri mbalimbali zitawakopesha mitaji inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya kila halmashauri.

Akizungumza kwenye Mahafali hayo ya 34, Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Profesa Hozen Mayaya, alisema Chuo chake kimepiga hatua kubwa katika masuala ya tafiti mbalimbali zinazogusa maendeleo ya Taifa na kuiomba Serikali iendelee kukiwezesha chuo hicho kufikia malengo yake ya kutoa elimu iliyotukuka katika Nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

“kutokana na umahili wa Chuo katika kufundisha kozi za muda mfupi na mrefu, idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa chuoni hapo imeongezeka akiitolea mfano wa mwaka wa masomo 2018/19 ambapo kwa Kampasi Kuu ya Dodoma peke yake wanafunzi wameongezeka kutoka 4,317 hadi kufikia wanafunzi 5,856 mwaka 2019/2020.

Profesa Mayaya alieleza kuwa Chuo chake kinatekeleza pia miradi kadhaa ya maendeleo ikiwemo mradi wa kuboresha ustahimilivu wa jamii za wafugaji na wakulima wa Serengeti ili kupunguza migogoro ya ardhi, mradi wa kuwajengea uwezo watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa Zanzibar, Mradi wa kuwajengea uwezo watumishi wa Wizara na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika uandaaji wa mipango ya bajeti inayozingatia mahitaji ya watoto.

Aliitaja miradi mingine kuwa ni Mradi wa kuandaa mipango mikakati Tanzania Bara ili kuwawezesha kufanya uchambuzi wa mahitaji ya watumishi na uandaaji wa mipango mikakati na mradi wa tathimini ya mbinu za upangaji wa mipango ya maendeleo na uhusishaji wa program ya program ya fursa na vikwazo katika mitaala ya vyuo vya elimu ya juu.

Alisema kiwango cha fedha kinachotumika kutoa mikopo kwa makundi mbalimbali wakiwemo vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalumu kimeongezeka kutoka shilingi bilioni 2 hadi shilingi bilioni 147 kwa mwaka.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Profesa Martha Qorro aliishukuru Serikali kwa kukipatia Chuo chake kiasi cha shilingi milioni 895 kwa ajili ya ujenzi wa hosteli ya wasichana yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 192 na kuongeza kuwa ujenzi wake utakapokamilika utatatua changamoto ya malazi ya wanafunzi hususan wa kike.

Aliiomba Serikali kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa hosteli hiyo pamoja na kuomba Chuo kiongezewe wahadhiri 81 wanaohitajika Chuoni hapo ili kukabiliana na upungufu wa wahadhiri ikilinganishwa na ongezeko la idadi ya wanafunzi ambapo hivi sasa Chuo kina wahadhiri 132 pekee.

Akizungumza kwa niaba ya wahitimu, mwanachuo Hemed Yassin Mussa, alisema kuwa wanafunzi waliohitimu wamejengewa uwezo wa kufanyakazi katika maeneo yote hususan ya vijijini na kwamba wako tayari kufanyakazi mahali popote watakapopangiwa ili kuwatumikiwa watanzania.

Chuo chas MIpango ya Maendeleo Vijijini kilianzishwa mwaka 1979 kwa Sheria Namba 8 ya Mwaka 1980 ikiwa chini ya Wizara ya Fedha na Mipango ya Fedha na Mipango ambapo lengo la kuanzishwa kwa Chuo hicho chenye tawi Jijini Mwanza ni kuandaa wataalam wa mipango ya maendelea hasa maendeleo vijijini.