NEWS

4 Septemba 2014

Baba Amnyonga Mtoto Wake na Kumzika Mwenyewe Kwenye Kibanda Chake

Mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi miwili , Regina Geofrey ameuawa kikatili kwa kunyongwa na baba yake mzazi Geofrey Kilngwa ‘Simbaiwe” (27) kwa kuwa alizaliwa akiwa ameatanguliza makalio yake .

Baba wa binti huyo ambaye pia ni mganga wa kienyeji anayeishi kitongoji cha Mwikang’ombe, kijijicha cha Katuma ,wilayani Mpanda alitenda unyama huo kwa madai kuwa mtoto aliyezaliwa kwa kutanguliza makalio yake ni mkosi na nuksi kubwa katika shughuli zake hizo za uganga wa kienyeji .

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi , Dhahiri Kidavashari akizungumza na waandishi wa habari amedai kuwa mzazi huyo aliyetenda uhalifu huo Julai 20 mwaka huu ambapo alikamatwa na jeshi la Polisi Agosti 26, mwaka huu..




Inadaiwa siku hiyo ya tukio mtuhumiwa huyo baada ya kumnyonga hadi kufa binti yake huyo alimzika kwa siri katika kibanda chake anachofanyia shughuli zake za uganga wa kienyeji .

Akisimulia mkasa huo Kamanda Kidavashari alidai kuwa mtoto Regina alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa ambao haukufahamika kwa zaidi ya mwezi mmoja .

“Ndipo baba mzazi wa binti huyo alipolazimika kuanza kumuuguza kwa siri pasipo mama yake mzazi kufahamu kwani alimdanganya kuwa mtoto wao huyo amepelekwa kutibiwa na babu yake huko mkoani Mwanza “ alieleza Kidavashari .

Inadaiwa kuwa kibanda ambacho mtuhumiwa alikuwa akifanyia shughuli zake za uganga kilikuwa mbali na makazi yake hivyo ilikuwa rahisi kumficha mtoto wake huyo kwa zaidi ya mwezi mzima akimtibu bila mama mzazi wa mtoto huyo kufahamu .

Kwa mujibu wa kamanda Kidavashari ,wakazi wa kitongoji cha Mwikan’gombe wakiongozwa na Mwenyekiti wao walimtilia shaka mtuhumiwa kutokana na tetesi zilizozagaa eneo hilo kuwa mtoto Regina alikuwa ameuawa na baba yake mzazi na kuzikwa kwa siri .

Inadaiwa wakazi hao na mwenyekiti wao waliamua kufika nyumbani kwa mtuhumiwa na kuhoji alipo binti yake Regina ambapo alipinga vikali lakini alipopekuliwa kibandani kwake walibaini kuweko kwa tuta dogo lililokuwa limechimbwa siku za karibuni .

Kidavashari aliongeza kuwa wakazi hao wakiongozwa na mwenyekiti wao waliamua kufukua tuta hilo na kukuta kichwa cha mtoto huyo kisha wakaitaarifu polisi .

Mama ya marehemu aitwae Maria Exavery (22) alidai kuwa hakuhusishwa wala kupewa taarifa kwamba binti yake huyo amekufa “Mie nilikuwa nafahamu kuwa Regina yuko kwa babu yake , Mwanza akitibiwa “ alieleza .

Nae Regina Kaboni (40) mkazi wa Isamilo Mwanza ambaye alikuwa akitibiwa na mtuhumiwa anadai kuwa alishirikishwa katika maziko ya binti huyo

“Hata hivyo nilishtushwa sana kwa kitendo cha mtuhumiwa kumzika mwanae bila ya kumshirikisha mkewe , nilipomuuliza mtuhumiwa alidai kuwa kwa mila ya kwao mtoto aliyezaliwa kwa kutanguliza makalio yake mama mzazi wa mtoto ni mwiko kushirikishwa katika maziko ya mtoto huyo ” anadai

Kwa mujibu wa Kidavashari watu wanne wakiwemo wazazi wa marehemu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi ambapo watafikishwa mahakamani mara tu baada ya upelelezi wa awa;li kukamilika ..

Wengine wanaoshikiliwa na Jeshi hilo ni pamoja na Regina Kaboni na Msolwa Jacob (29) mkazi wa kitongoji cha Mwikanga’ombe .