NEWS

16 Septemba 2014

Mwanamuziki Chaz Baba Nusura Amuue Mkewe, Ampiga mkewe Mpaka Mke Kuzimia

PREZIDAA wa Bendi ya Mashujaa Musica, Charles Gabriel Mbwana ‘Chaz Baba’ anadaiwa nusura amtoe roho mkewe wa ndoa, Rehema Sospeter Marwa baada ya kumpiga na kitu kizito kichwani mpaka kushonwa nyuzi ishirini.

MANENO YA CHANZO
Kwa mujibu wa chanzo chetu makini ambacho kipo karibu na wanafamilia hao (jina limehifadhiwa), usiku wa Alhamisi iliyopita, kikiwa maeneo ya Kinondoni jijini Dar kilishuhudia ugomvi huo baada ya kwenda kuangalia nani anamshushia kipondo mwenzake.



Chanzo kilisema baada ya kufika, ndipo kiligundua kuwa, mwanamuziki huyo ndiye aliyekuwa akimpa kipondo mke wake.

“Dah! Kiukweli kile si kipigo cha kumpiga mke, hasira bwana ni kitu cha ajabu sana. Chaz anatakiwa kujiangalia sana,” kilidai chanzo hicho.

MKE AFUNGUKA ‘EI TU ZEDI’
Baada ya taarifa hiyo, juzi Ijumaa Wikienda lilimtafuta mwanamke huyo ili aeleze nini kilitokea hadi mumewe kutaka kumkatishia maisha.“Nakumbuka siku ya tukio nilikuwa supermarket maeneo ya Mwananyamala A (jijini Dar) nikinunua unga wa ulezi wa mtoto, ghafla Chaz alitokea, akaniamuru niingie kwenye gari alilokuwemo, tukaondoka kuelekea nyumbani.

“Tulipofika maeneo ya Kinondoni, pale Meridian ndipo niliposhtukia naanza kupigwa. Nakumbuka nilipigwa hadi nikaishiwa nguvu mpaka akatokea rafiki wa Chaz, Hassan Kisanora na kuniokoa, nikakimbilia nyumbani,” alisema mwanamke huyo.

CHAZ ATOWEKA, ARUDI NA SAMAKI MKUBWA
Akiendelea kuzungumza, mke huyo alisema: “Siku hiyo Chaz aliondoka na hakurudi nyumbani mpaka alfajiri. Aliporudi aliniambia amekuja na samaki mkubwa, yuko kwenye friji huku akisahau kuwa amenikosea na anatakiwa kuniomba msamaha.

“Sikumjibu, ndipo alipochukua kitu kizito na kunipiga nacho kichwani, baada ya hapo damu nyingi zikaanza kunitoka hadi puani, niliishiwa nguvu na kupoteza fahamu.”
“Nilipokuja kuzinduka nilikuwa hospitali kwa Dk. Mvungi, Kinondoni. Licha ya kwamba nampenda sana lakini alitaka kuniua, hata sijui kisa.”

MADAI YA KUSHANGAZA; NDANI YA MIEZI TISA KICHAPO MARA 16
Katika kuweka mambo zaidi hadharani, mwanamke huyo aliyebahatika kupata mtoto mmoja na mumewe, alikwenda mbele zaidi kwa kusema kuwa, tangu afunge ndoa na Chaz miezi tisa iliyopita, ameshachezea kichapo mara kumi na sita hivyo amechoka kufanywa ngoma.“Nimechoka kufanywa ngoma na Chaz, ndoa ina miezi tisa tu nishapigwa mara kumi na sita kati ya hizo nimezimia mara saba kama vipi bora afanye utaratibu anirudishe kwetu,” alimalizia kusema.

CHAZ BABA, IJUMAA WIKIENDA
Baada ya kupata maelezo ya mke, Ijumaa Wikienda lilimsaka kwa njia ya simu Chaz mwenyewe ili azungumzie ishu hiyo ya mkewe kudai alimpiga ambapo alipopatikana alifunguka hivi:
“Ni wivu tu kaka! Unajua mke wangu ana wivu mkali sana, alianza kunipiga yeye mimi ndiyo nikamrudishia, hakukuwa na sababu nyingine yoyote zaidi ya wivu,” alisema Chaz bila kufafanua.

Stori: Shakoor Jongo
GPL