NEWS

29 Desemba 2016

Ushahidi uliotolewa Mahakamani juu ya kesi inayomkabili ‘Scorpion’

Mashahidi wawili katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kujeruhi inayomkabili, Salum Njwete ‘Scorpion’, wameieleza Mahakama ya Wilaya ya Ilala kuwa mlalamikaji Said Mrisho alimtaja Scorpion kwamba ndiye aliyemchoma visu na kumtoboa macho.

Waliotoa ushahidi jana ni mke wa Mrisho, Stara Sudi, shahidi wa pili katika kesi hiyo na Yahaya Kisukari ambaye ni mdogo wake Mrisho. Walidai hayo mbele ya Hakimu Mkazi, Flora Haule.

Awali, akitoa ushahidi huo, Stara alidai Septemba 6 mwaka huu, majira ya saa 5 usiku akiwa amelala, alisikia simu inaita ambayo ilikuwa ni namba ngeni na baada ya kuipokea alisikia sauti ya mume wake aliyemtaarifu kuwa yupo Buguruni amechomwa visu na kuona haoni.

Akiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Nassoro Katuga, shahidi huyo alidai kuwa baada ya kupokea simu hiyo, ilikatika kisha simu ikaita tena ambapo msamaria mwema alimwambia kuwa hali ya mume wake sio nzuri na kwamba wanaelekea Hospitali ya Amana.

“Baada ya taarifa hizi nilimwambia mwanangu Abdul (12), kwamba baba yake anaumwa hivyo naenda kwa bibi yake kumpa taarifa. Nilipanda pikipiki hadi Mabibo Hostel kwa wazazi wa mume wangu ambako tuliondoka kuelekea hospitali; njiani nilimpigia shemeji yangu Kisukari kumpa taarifa hizo,’’ alidai Stara.

Aliendelea kudai kuwa walipofika Amana walimkuta Mrisho akiwa amelazwa wodini huku amefungwa bendeji usoni, mgongoni na tumboni na kwamba nguo zake zilikuwa zimelowa damu.

Pia alidai kuwa dokta alimtaka akanunue mpira wa mkojo, na wakati akimbadilisha nguo alizungumza naye na kumwambia mkasa huo; kwamba alivamiwa na kuchomwa visu na alipopiga kelele hakuna aliyejitokeza kumsaidia.

Stara alidai kuwa walipewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ambapo shemeji yake Kisukari na Mrisho walitumia gari la wagonjwa kwenda hospitalini hapo alikofanyiwa upasuaji tumboni na baada ya vipimo vya macho iligundulika hataweza kuona tena.

“Huku nikishughulika na masuala ya hospitali, nilikwenda Kituo cha Polisi cha Buguruni ambako walichukua maelezo na kunieleza kuwa suala la mtu aliyemjeruhi mume wangu niwaachie,’’ alidai shahidi huyo.

Naye Kisukari alidai kuwa alikuwa anafanya kazi pamoja na kaka yake katika saluni inayoitwa Rodgers iliyopo Tabata Saanene. Alidai kuwa kaka yake alimtajia mtu aliyemchoma visu tumboni, mgongoni na machoni.

– Habari Leo

The post Ushahidi uliotolewa Mahakamani juu ya kesi inayomkabili ‘Scorpion’ appeared first on SWAHILI TIMES.