NEWS

8 Juni 2017

WADAU WAKUTANA KUJADILI MFUKO WA KUENDELEZA UBUNIFU VIJIJINI

Wadau kutoka sekta za kilimo na uchumi wamekutana kujadiliana namna bora ya uanzishwaji wa Mfuko wa Ubunifu Vijijini (rural innovation fund) wenye lengo la kuchochea, kuhamasisha na kusaidia uvumbuvi katika maeneo ya maendeleo vijijini, ukopeshaji wa shughuli za kilimo na huduma za taasisi ndogo za kifedha.

Mkutano huo wa siku moja umeandaliwa kwa ushirikiano wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani Mazao na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF).

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Adam Kamanda amesema wadau wana mchango mkubwa wa kutoa maoni yatakayosaidia kuboresha usimamizi wa Mfuko huo ambao utakuwa chini ya TADB.

“Nawaomba tujadili namna bora itakayosaidia ndoto ya Serikali ya kuchagiza upatikanaji wa fedha za gharama nafuu kwa ajili ya kuwasaidia wakulima hasa katika maeneo ya maendeleo vijijini, ukopeshaji wa shughuli za kilimo na huduma za taasisi ndogo za kifedha,” alisema.

Bw. Kamanda ameongeza kuwa uanzishwaji wa mfuko huu unalenga kutekeleza kwa vitendo dhamira ya Serikali ya kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo ambayo ni shughuli kuu kwa Watanzania wengi wanaoishi maeneo ya vijijini.
Mratibu wa Uanzishwaji wa Mfuko wa Ubunifu Vijijini, Bw. Albert Ngusaru akizungumza kabla ya ufunguzi wa mkutano wa siku moja wa kujadili namna bora ya kuendeleza Mfuko huo.
Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Adam Kamanda (kushoto) akifungua mkutano wa siku moja wa kujadili namna bora ya kuendeleza Mfuko wa Ubunifu Vijijini huo.
Washiriki wa Mkutano wa Majadiliano ya Uanzishwaji wa Mfuko wa Ubunifu Vijijini wakifuatilia kwa umakini mkutano huo.