SIKU chache baada ya Zarinah Hassan ‘Zari Boss Lady’ kuweka wazi kuwa ameachana na baba watoto wake, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, swali linakuja ni kwa nini Zari anaweza kuwa ameumizwa sana na Wema Abraham Sepetu na si Hamisa Mobeto ambaye hivi karibuni amempa msongo wa mawazo baada ya kuzaa na baba watoto wake? Twende taratibu!
Kwanza nauliza swali hilo ambalo nitaliweka wazi baadaye kidogo na kadiri unavyoendelea kusoma makala haya, utanielewa.
Baada ya matukio yote ya Diamond na Mobeto, bado Zari alionekana kuwa ‘jiwe’ na kutetea penzi lake lakini lilipokuja suala la shoo ya Mboso ambayo Diamond alionekana wazi kuwa na mahaba na Wema kwa video yao ya ‘kupapasana’ kuwekwa mitandaoni, siku chache baadaye Zari aliamua kutangaza rasmi kummwaga Diamond.
Sababu ya wadau na mashabiki wa Baba Tiffah na Mama Tiffah kuona kuwa hiyo itakuwa imemuudhi Zari ni jinsi wapendanao hao walivyopotezeana hata kabla ya Zari kutangaza kuachia ngazi na muda mwingi akaonekana kuutumia kwenda kanisani na kwenye mihadhara ya kidini akiwa ameongozana na wanawe.
Zipo sababu nyingi ambazo zinaweza kuwa zimechangia Zari kuumizwa zaidi na Wema lakini si vibaya nikikutajia zifuatazo:
NGUVU YA WEMA KWENYE JAMII
Wema ana jina kubwa kwenye jamii, ana ushawishi na yeye akiamua kufanya kazi na Diamond ni rahisi sana kuwateka watu na bado mambo yakawaendea vizuri.
Zari anaifahamu nguvu ya Wema na ndiyo maana anaona endapo akiamua kushindana naye, atapoteza muda wake bure wakati ana mambo mengi ya kufanya ikiwa ni pamoja na kusaka pesa na kulea watoto.
WEMA NDIYE ‘ROHO’ YA DIAMOND
Zari anajua wazi kuwa Wema ndio kipenzi cha moyo wa Diamond kwa sababu amewahi kukiri kwake kuwa alimuumiza kama alivyosimulia kwenye mahojiano yake na vyombo vya habari nchini Uganda hivi karibuni.
Zari alieleza kuwa, wakati wanaanza uhusiano wao, Diamond aliwahi kumueleza jinsi alivyoumizwa na mapenzi na kudharaulika lakini pia alikuwa akitaka mtoto kwani wasichana wengi wameshindwa kuzaa naye, Zari akaamua kumpa nafasi moyoni mwake kisha akamzawadia watoto.
WEMA NI BIDHAA ADIMU
Kwa ‘brand’ yake ya Miss Tanzania, Wema anaweza kuuzika nchi yoyote kama atapata mameneja wazuri kwani hata lugha kwake si ya kujifunza lakini pia alishaiteka jamii tofauti na Hamisa ambaye pamoja na uanamitindo wake hashtui sana na hawezi kushindana na Zari.
WEMA ANA MVUTO
Wema ana mvuto pia wa sura. Ana shepu matata ambayo kwa warembo wengi wa Kibongobongo ni nadra sana kuwa kama yeye. Hilo limempa pia hofu Zari ya kupambana naye kuliko Mobeto ambaye alifikia hadi levo ya kuzaa na Diamond. Utakubaliana na mimi kwamba, kwa shepu Zari hamfikii Wema.
NI MWANAMKE ALIYEMNYANG’ANYA DIAMOND
Jambo lingine linalomfanya Zari amhofie zaidi Wema kuliko Mobeto ni kwa sababu mrembo huyo alimchukua Diamond akitokea kwa Wema. Zari anatambua fika kwamba katika uhusiano ambao ulikuwa ‘strong’ wa Diamond, wa Wema ndio ulishika namba moja.
NGUVU YA WEMA KWA FAMILIA
Licha ya Diamond kuwakaribisha warembo wengi kwenye familia yake akiwemo mtangazaji Penniel Mungilwa ‘Penny’ na Jokate Mwegelo, Wema anamuuma zaidi Zari kwa sababu anafahamu pia jinsi familia ya Diamond inavyomkubali Wema.
Anafahamu ‘mahaba’ ya wazi ya mama mzazi wa Diamond kwa Wema, anafahamu jinsi dada yake Diamond, Esma Platnumz anavyomhusudu Wema tofauti hata na Mobeto.
Usihau, hata baba yake Diamond, Mzee Abdul Jumaa, mara kadhaa amewahi kutamka kuwa anamkubali sana Wema kwani ndiye mwanamke pekee aliyewahi kufika nyumbani kwake.
Makala: Hamida Hassan
The post KWA NINI ZARI KAUMIZWA NA WEMA NA SI MOBETO? appeared first on Global Publishers.