
Waandamanaji wakiongozwa na viongozi wa Kanisa Katoliki nchini DR Congo.
Mahakama kuu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, imemhukumu kifungo cha maisha askari polisi aliyewafyatulia risasi waandamanaji wanaompinga na kumtaka kujiuzulu Rais wa nchi hiyo, Joseph Kabila.
Polisi huyo aliwapiga risasi za moto waandamanaji wawili na kuwaua Jumapili iliyopita, Februari 25, na kuibua hisia kali kwa raia wa Congo baada ya video yake kusambaa mitandaoni.
Waumini wa Kanisa Katoliki wakiongozwa na viongozi wao waliandamana katikati ya jiji la Kinshasa wakishinikiza Rais Joseph Kabila ang’atuke madarakani.
Kwa mujibu wa mtandao wa Frontline Defenders, Shirika ambalo linafanya kazi chini ya mwavuli wa Haki za Binadamu, ni kuwa mpaka sasa zaidi ya watu 35 wanaoandamana kushinikiza Rais Kabila kujiuzulu wameuawa na polisi nchini DR Congo.
Hata hivyo shirika la Haki za Binadamu bado linadai hukumu hiyo haijatenda haki sawasawa kwani imewaacha wakuu wa jeshi la polisi bila kuwagusa.
Chanzo: Frontline Defenders
The post Polisi DR Congo Afungwa Maisha Kwa Kuua Waandamanaji appeared first on Global Publishers.