NEWS

30 Desemba 2016

Mfahamu Profesa mwenye asili ya Tanzania aliyepewa uongozi na Rais Kagame

Silas Lwakabamba ni Profesa wa masuala ya Sayansi na Teknolojia nchini Rwanda aliyezaliwa mwaka 1947 mkoani Kagera nchini Tanzania (Tanganyika wakati huo).

Silas Lwakabamba alizaliwa nchini Tanzania na kupatia sehemu ya elimu yake nchini Tanzania. Elimu ya msingi alisoma huko Muleba mkoani Kagera na kisha akajiunga na Shule ya Sekondari ya Ihungo. Baada ya hapo alikwenda katika Chuo Kikuu cha Leeds nchini Uingereza ambapo alihitimu mwaka 1971 na kutunikiwa Shahada ya Awali ya Uhandisi wa masuala ya Sayansi na Teknolojia na mwaka 1975 alitunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD).

Baada ya hapo alirejea nchini Tanzania na kufanya kazi katika Kitivo cha Uhandisi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Silas Lwakabamba alitunukiwa Uprofesa mwaka 1981. Baada ya muda mfupi aliteuliwa kuwa Mkuu (Dean) wa kitivo hicho.

Mwaka 1977, Prof. Lwakabamba alikuwa Mkuu wa Kwanza wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Kigali (KIST) nchini Rwanda na kuiongoza hadi ilipofika mwaka 2006 ambapo aliteuliwa kuwa Gombera wa Chuo Kikuu cha Rwanda, taasisi kubwa zaidi ya elimu ya juu nchini Rwanda.

Prof. Lwakabamba alishikilia nafasi hiyo hadi mwaka 2013 alipoteuliwa kuwa Waziri wa Miundombinu katika Baraza la Mawaziri nchini Rwanda. Ilipofika Julai mwaka 2014, Prof. Lakwabamba aliteuliwa na kuwa Waziri wa Elimu wa Rwanda hadi Juni 24, 2015.

Msomi huyo alikwenda  nchini Rwanda na kuchukua uraia wa nchi hiyo mwaka 1997, baada ya kuombwa na Paul Kagame ambaye alikwenda UDSM kuwaomba baadhi ya wahadhiri kwenda Kigali kufungua Chuo Kikuu katika taifa hilo baada ya kumalizika vita ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1994.

Profesa Lwakabamba amelazimika kuukana uraia wa Tanzania kwa kuwa katiba ya nchi hairuhusu uraia wa nchi mbili.

Prof. Lakwabamba ameoa na ana watoto wanne.

The post Mfahamu Profesa mwenye asili ya Tanzania aliyepewa uongozi na Rais Kagame appeared first on SWAHILI TIMES.