NEWS

19 Februari 2018

Ripoti Kifo cha Akwilina Kizungumkuti

Mkuu wa Chuo cha NIT, Zakaria Mganilwa.

 

RIPOTI maalum kuhusu kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini imezua kizungumkuti katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ulipohifadhiwa baada ya baadhi ya ndugu wa marehemu kuelezwa kuwa majibu ya ripoti hiyo yatatolewa baada ya siku 14 kuanzia leo Februari 19, 2018.

 

Wakizungumza na Global TV Online, ndugu wa Akwilina wameeleza kusikitishwa kwao na uamuzi huo huku wakilalamika na kuhoji kwa nini wasipewe ripoti hiyo leo ili wakazike mwili wa ndugu yao.

 

“Tumeambiwa na daktari tayari uchunguzi umeshakamilika, tuchukue mwili tukazike, lakini wanasema majibu yatatoka baada ya siku 14. Hivi tukienda tukizika tutawaambiaje waombolezaji na ndugu wengine, kwamba ndugu yetu alikufa je?” alisema ndugu mmoja ambaye hakutaka kutaja jina lake litajwe.

 

Hali hiyo ilizua sintofahamu huku wengine wakikubali kuchukua mwili na wengine wakikataa wakitaka kupewa ripoti kamili ya uchunguzi wa kifo hicho. Mpaka tunaenda mitamboni bado mjadala wa kuchukua  mwili huo ulikuwa unaendela Muhimbili na majibu yalikuwa hayajapatikana.

 

Kwa upande wa Mkuu wa  NIT, Zakaria Mganilwa amesema uongozi wa chuo hicho umeungana na familia kuhakikisha wanampumzisha Akwilina huku akifanya jitihada za kuzungumza na madaktari na ndugu wa marehemu kufanikisha zoezi la kuchukua mwili na kwenda kuuzika.

The post Ripoti Kifo cha Akwilina Kizungumkuti appeared first on Global Publishers.