NEWS

21 Februari 2018

Wakati Kifo cha Akwilina Kikitikisa, Mfanyabiashara Auawa Nje ya NIT

Paulo Kaguo enzi za uahi wake.

 

WAKATI kifo cha denti wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini kilichotokea baada ya kupigwa risasi kwenye maandamano ya Chadema maeneo ya Kinondoni- Mkwajuni jijini Dar akiwa ndani ya daladala kikitikisa, juzikati mauaji tena ya mfanyabiashara yametokea nje ya chuo alichokuwa akisoma mwanafunzi huyo, Risasi Mchanganyiko linakupa habari kamili.

 

Taarifa za awali zilieleza kwamba juzikati majira ya saa sita mchana mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la Paulo Kaguo, mkazi wa Mabibo-Jitegemee alikutwa ameuawa nje ya chuo hicho cha NIT.

“Jamani kuna mtu ameuawa hapa nje ya Chuo cha NIT na anaonekana ana jeraha kama la kisu tumboni mwake ambapo damu nyingi imetapakaa eneo mwili ulipo huku kisu kikiwa pembeni yake,” alidai mtoa habari huyo aliyeomba asitajwe jina lake gazetini akiogopa kulisaidia Jeshi la Polisi.

 

Akwilina Akwilini enzi za uhai wake.

 

Risasi Mchanganyiko lilifika maeneo ya Mabibo na kufanikiwa kukutana na askari mmoja ambaye naye hakutaka jina lake liandikwe gazetini kwa kuwa si msemaji wa polisi ambaye alieleza kuwa mtu huyo anadaiwa amejiua mwenyewe kwa kujichoma kisu tumboni tofauti.

“Taarifa zilizosambaa ni kwamba yule mtu ameuawa pale nje ya kile chuo lakini inavyoonekana kajiua mwenyewe kwa kujichoma kisu. Ilikuwa majira ya saa nne asubuhi ambapo taarifa hizo zilienea ambapo polisi walifika na kuukuta mwili wa jamaa huyo ukiwa umelala huku macho yakiwa wazi na jeraha tumboni huku kisu kikiwa pembeni.

 

“Shuhuda mmoja alidai alishuhudia mwanaume huyo akijichoma kisu mwenyewe mpaka anakata roho kutokana na damu nyingi kumtoka.

“Polisi waliuchukua mwili na baada ya hapo ndipo ndugu wakaanza kutafutwa kwa bahati wakapatikana na kwenda kuutambua mwili kwamba ni wa ndugu yao,” alisema askari huyo.

 

Kondakta wa gari alimokuwa Akwilina siku ya umauti wake.

 

RISASI LATINGA ALIKOKUWA ANAISHI

Ili kupata ukweli wa habari hiyo, Risasi Mchanganyiko lilifika nyumbani alikokuwa anaishi kijana huyo na kukutana na mmoja wa ndugu aliyekuwa akiishi naye aliyejitambulisha kwa jina moja la Flora na kueleza kuwa ni kweli walipata taarifa kutoka kwa polisi kuhusu ndugu yao huyo.

 

“Marehemu Paulo ni ndugu yangu yaani ni kabila moja na mimi, siku ya tukio alitoka nyumbani asubuhi kwenda kazini kama kawaida kwani anafanya biashara kwenye soko la viazi hapo Mabibo na hakuwa na tatizo lolote.

“Ilipofika saa sita mchana walikuja watu ambao walijitambulisha kuwa ni polisi wakiwa na picha ikimuonyesha Paulo akiwa amelala na kusema kwamba wamemkuta akiwa amefariki hivyo twende eneo la tukio tukamtambue kama ni yeye.

 

Dereva wa gari hilo.

 

“Tulienda eneo la tukio ambalo ni nje ya chuo cha usafirishaji karibu na bandari kavu ambapo tulimtambua kweli kwamba ni yeye akiwa ana jeraha tumboni kwenye kitovu huku kisu kikiwa pembeni ya tumbo.

“Kwa jinsi tulivyoelezwa na mashuhuda wa tukio hilo walisema walimwona akijichoma mwenyewe kisu tumboni lakini hatujajua ni kweli kajichoma au kachomwa. Na kama kajichoma ni kwa nini alifanya hivyo kwa sababu alitoka nyumbani akiwa hana shida yoyote na hakuwa hata na ugomvi na mtu yeyote,” alisema Flora.

 

MSIKIE JIRANI

Mmoja wa majirani wa Paulo aliyejitambulisha kwa jina la Saidi alisema kuwa, wana shaka na kifo cha ndugu yao huyo kwani haiwaingii akilini kwamba kajiua mwenyewe.

“Tumeambiwa amejiua lakini pia kuna uwezekano kuwa kauawa, unajua lolote linaweza kuwa limetokea. Ila jamani kifo cha huyu jamaa kimetuuma sana, alikuwa mtu poa sana, alikuwa akipenda kila mtu ila ndo hivyo mwisho wa maisha yake umefika,” alisema Saidi.

 

Kamanda wa Polisi Dar, Lazaro Mambosasa.

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Muliro Jumanne Muliro alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo alisema hana taarifa hizo.

“Hiyo habari ndiyo kwanza naisikia kwako wewe mwandishi, sijapata taarifa bado,” alisema Kamanda Muliro.

Alipotafutwa Mkuu wa Chuo cha NIT, Prof. Zacharia Mganilwa kuhusiana na tukio hilo alisema hawezi kulizungumzia kwa kuwa limetokea nje ya chuo chake.

“Hiyo labda uende polisi Urafiki maana hiyo ni ishu ya kipolisi na ni nje ya chuo chetu,” alisema Prof. Zacharia.

 

Mkuu wa Chuo cha NIT, Prof. Zacharia Mganilwa.

 

NDUGU WA AKWILINA SASA

Kwa upande wa Akwillina, hadi tunakwenda mitamboni, ilielezwa kuwa baadhi ya ndugu wa marehemu walikuwa wakikomaa kutaka kumjua aliyempiga risasi ndugu yao ili kuhakikisha anachukuliwa hatua stahili lakini wengi walisema kuwa, itampendeza Mungu

kwenda kumhifadhi mpendwa wao kwanza kisha mengine yatafuata.

 

“Kwa kweli licha ya kwamba ndugu wengi wameshakubali kuuchukua mwili na kwenda kuzika, bado kuna baadhi wanataka tu kumjua muuaji na wameapa kwamba lazima sheria ichukue mkondo wake,” alisema mmoja wa wanafamilia.

Marehemu Akwilina anatarajiwa kuzikwa kijijini kwao, Marangu Utowo, wilayani Rombo Mkoani Kilimanjaro ambapo kutokana na jinsi kifo chake kilivyowagusa wengi wa vyama vyote, ni lazima mazishi yake yatatikisa nchi.

Mungu ailaze roho ya marehemu Akwilina mahali pema peponi, Amina.

STORI: Mwandishi Wetu, Risasi Mchanganyiko | DAR ES SALAAM

 

KWA STORI KAMA HIZI, ZINAPATIKANA KWENYE APPLICATION YA GLOBAL PUBOLISHERS

Install

Android: ==>

iOS: ==>

The post Wakati Kifo cha Akwilina Kikitikisa, Mfanyabiashara Auawa Nje ya NIT appeared first on Global Publishers.