WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya ya Misungwi Bw. Alphonce Sebukoto na kuagiza achungunzwe na vyombo husika.
Amechukua hatua hiyo baada Mwanasheria huyo kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwa ni pamoja na kushindwa kuishauri vema halmashauri hiyo na kuisababishia hasara ya sh. milioni 279.
Waziri Mkuu amemsimamisha kazi Bw. Sebukoto leo (Jumatatu, Februari 19, 2018) wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa halmashauri hiyo akiwa katika siku ya tano ya ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.
“Mwanasheria utasimama kazi kuanzia leo na tuhuma zako zitachunguzwa kikamilifu na vyombo husika na uchunguzi ukibaini kama huna kosa utarudi kazini. Hatuta kuonea lakini hatuwezi kukuvumilia kwa utaratibu huo ulioufanya.”
Amesema mwanasheria huyo Novemba 2017 wakati alipokuwa anakaimu nafasi ya ukurugenzi aliidhinisha malipo ya sh.milioni 279 zilipwe katika akaunti binafsi ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Bw. Anthony Bahebe.
Waziri Mkuu amesema Bw. Bahebe aliishtaki halmashauri hiyo akidai kulipwa fedha kwa ajili ya kazi ya ukandarasi wa mradi wa maji Igenge uliojengwa na kampuni ya ukandarasi ya Seekevim.
Amesema mradi huo ulianza 2014 na ulitakiwa ukamilike 2015. Mwanasheria huyo aliidhinisha malipo hayo wakati ambao tayari hati maalumu ya uwakilishi ilikuwa imekwisha tangu Desemba 2015.
“Mwanasheria amemlipa Mwenyekiti wa Halmashauri kwa kufanya kazi na Halmashauri baada ya kuifikisha Halmashauri yake Mahakamani. Amemlipa fedha wakati kazi yenyewe ilikuwa haijaisha na aliharakisha malipo hayo kipindi ambacho Mkurugenzi hayupo.”
Waziri Mkuu amewakumbusha watumishi wa umma kuzingatia maadili ya utumishi na matakwa ya kisheria katika utekelezaji wa majukumu yao. Amesema fedha alizolipwa Bw. Bahebe zingeweza kutumika katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri hiyo.
Awali, Waziri Mkuu alifungua mabweni ya watoto wenye mahitaji maalumu katika shule ya msingi Mitindo iliyoko wilayani Misungwi na kisha alikagua ujenzi wa vyumba vya madarasa.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, FEBRUARI 19, 2018.