NEWS

24 Februari 2018

Yanga SC Yaifuata Majimaji Kwa Ndege

Kikosi cha timu Ya Yanga.

KIKOSI cha wachezaji 20 wa Yanga na viongozi wao leo asubuhi wanatarajiwa kusafiri kwa ndege kwenda Songea tayari kwa mechi yao ya kesho Jumapili ya 16 Bora ya Kombe la FA dhidi ya Majimaji FC.

 

Yanga inakwenda Songea ikiwa ni siku moja tu tangu iliporejea kutoka Victoria, Shelisheli ambako ilikwenda kucheza na St Louis mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambako walitoka sare ya bao 1-1.

 

Hata hivyo, Yanga imesonga mbele katika michuano hiyo ya Afrika kwa ushindi wa jumla ya mabao 2-1, kwani katika mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam ilishinda bao 1-0.

Kikosi cha timu ya Majimaji.

Yanga ilitinga hatua ya 16 bora ya Kombe la FA baada ya kuiondoa Ihefu FC ya Mbeya kwa penalti 4-3 baada ya kutoka sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh alisema: “Tunaondoka kesho (leo) saa 4:00 asubuhi kwenda Songea na ndege ya Air Tanzania (Bombardier) baada ya mazoezi.

“Lengo la kusafiri na ndege ni kuhofia wachezaji wetu kupata uchovu wa safari kwani Songea ni mbali na kama tukitumia basi wachezaji watachoka na kushindwa kucheza kwa ufanisi.

 

“Ratiba inatubana kiukweli, angalia jana (juzi) timu ilirejea saa nne usiku ikitokea Shelisheli na leo (jana) tulifanya asubuhi mazoezi mepesi kwa muda mfupi kwa hofu ya kuwachosha wachezaji wetu.

 

“Baada ya mazoezi tunawapumzisha wakijitayarisha kwa ajili ya safari ya kesho (leo) asubuhi tutakaposafiri saa nne asubuhi, utaona ni jinsi gani ratiba inavyotubana na kushindwa kufanya maandalizi ya kutosha.”

 

Saleh alisema majeruhi wa timu hiyo wanaendelea vizuri akiwemo Juma Mahadhi aliyeugua ghafla homa akiwa Shelisheli na yupo katika msafara utakaoenda Songea.

 

“Wachezaji wengine kama (Donald) Ngoma, (Amissi) Tambwe, (Thabani) Kamusoko na (Obrey) Chirwa wenyewe bado wanaendelea na matibabu,” alisema Saleh.

The post Yanga SC Yaifuata Majimaji Kwa Ndege appeared first on Global Publishers.