
THROUGH Back Thursday (TBT), ni ‘trend’ ambayo ipo kwenye mitandao ya kijamii hasa Instagram, Facebook na Twitter ambapo watu huposti ‘content’ za kitambo ambazo ni pamoja na picha au video, enzi za utotoni, katika makuzi yao ya ujana, zama wanazokumbuka huku wakiambatanisha ‘hash tag’ inayosomeka #TBT’.
TBT huwa ni maalumu katika siku ya Alhamisi (Thursday), ambapo haina tofauti kimantiki na ‘Flashback Friday’.
Sasa ukiachana na TBT, hiyo ya kwenye mitandao ya kijamii, kwenye Muziki wa Bongo Fleva pia tuna ngoma zinazotengeneza TBT ya kibabe. Hizi ni ngoma kali zilizotungwa na kufanywa na wanamuziki wenye uwezo mkubwa ambazo mpaka leo ukizisikiliza hakika zitakukosha.
Hapa tunazungumzia mwanzoni mwa miaka ya 2000 mpaka katikati mwa miaka hiyo. Ngoma hizo zipo nyingi, lakini zifuatazo ni baadhi yake;

TID na Gilfriend
Mnyama fl’an hivi anapatikana kwenye ‘mbuga’ za Kinondoni. Anaitwa Khaleed Mohamed ‘TID’ ambaye ngoma yake ya Gilfriend, aliyoshirikiana na Jay Moe ni miongoni mwa TBT za Kibabe. Ukisikiliza ngoma hii hakika mpaka leo inaishi. Kwanza mistari ya Jay Moe, ni hatari pale anapomuelezea mrembo anayemtafuta. Anakwambia;
“Ukimuona utamuona nacho, siyo mpenda makuu, ni mwenye tofauti kubwa, kuanzia chini mpaka juu, mtoto ana mapozi, kiboko ya masista du, na kila nikimtazama nazidi kumpenda tu. Aaah! Sisemi mengi, but I wanna be your boyfriend, hakuna zaidi yako please be my girlfriend, uwe wangu wa kufa na kuzikana mama…!”
Hapo mrembo atachomoa kweli! Sasa huyo ni Jay Moe, msikilize TID naye, anakwambia;
“Yaani picha limeanza, Top in Dar nimepigika, kwa kifupi natafuta, dada mwenye vyangu vigezo, kwanza, akitembea kama kinyonga, pili, awe anaringa kama twiga, nadhani hapo umenipata msela wako nakupa da…da…daataaaa…!”

Abdul Sykes ‘Prince Dully Sykes.”Mista misifa sasa!
Ukiachana na TID na Jay Moe ambao kabla ya Gilfriend walishawahi kukutana tena kwenye ngoma iitwayo Zeze, nakudondosha mpaka Kariakoo, kwa kijana mpenda sifa, ‘handsome boy’, Abdul Sykes ‘Prince Dully Sykes.”
Dully listi yake ya TBT ya kibabe ipo full. Unaanza na Julieta, halafu unakuja kwa Nyambizi, demu aliyekutana naye alipokwenda kumtembelea mshikaji wake Eddy Kazi, kwenye yake kazi ya ulinzi, hukoooooo Tangi Bovu na akamkumbusha walivyokutana siku ya Valentine. Achana na hizo sasa sikia Ladies Free, Leah dah huyu jamaa muache tu kama alivyo!

‘Mr Nice’ Kuku akapandishwa baiskeli
Huku kina TID, Dully Sykes wakihangaika na warembo, Lucas Mkenda ‘Mr Nice’, mhasisi wa staili ya Takeu (Tanzania, Kenya na Uganda), aliibuka na kumpandisha kuku baiskeli kisha bata akamvalisha raizoni.
Hapa nazungumzia ngoma yake ya Fagilia iliyomtam-bulisha vyema kwenye gemu. Kisha baadaye Kikulacho, Kidali Poo na nyingine kibao zinatengeneza TBT ya kibabe.

‘Juma Nature ‘ Mzee wa busara noma!
Pande za uswazi, Mitaa ya Temeke, tunakutana na mkali Juma Nature ambapo anamchana Mzee wa Busara, mzee wa ndumba, juju, mtu wa kuwangawanga!
Sasa achana na ngoma hiyo ya Mzee wa Busara, sikiliza Staki Demu. Nature hapa anamkazia demu na anasema sitaki demu kwa herufi kubwa huku akimwambia;
“Nakuomba usije kwetu mam’dogo utatutia hasara, huyo mdogo wangu mwenyewe tu katoka shule hajala.” Ilimradi amekwisha pima na amejikuta hana ngoma…sasa demu wa nini! Atambae zake hamtishi kwa lolote!
Nature ana TBT kali sana. Baadhi yake ni Kisa Demu na Hili Gemu. Baadaye aliua zaidi alipoungana na wenzake kina Temba, Chege na kuanzisha Kundi la TMK Wanaume Familly.
Mandojo na Domo Kaya
Washikaji hawa sauti zao ni za dhahabu usipime. Unakumbuka ngoma yao ya Wanok Nok wakiwa na Lady Jaydee? Ni ngoma kali ambayo hakika haipaswi kukosekana kwenye listi hii ya TBT, maana katika ngoma hii wanafiki walipewa za chembe na mtaani ilitengeneza headlines za kumwaga.
Inspector Haroun
Huyu jamaa naye alifanya vizuri sana. Ngoma zake za Asali wa Moyo, Byee Byeee na hata akiwa na kundi lake la Gangwe Mob, ngoma ya Mtoto wa Geti Kali, iliweza kufanya vizuri sana.
Professor Jay, Afande Sele na Solo Thang
Washikaji hawa waliumana vilivyo kwenye shindano la kumtafuta Mkali wa Rhymes Bongo na wote walitikisa kwa ngoma kali! Ukianza na Professor Jay, kipindi hicho alikuwa anakimbiza mbaya na ngoma zake za Msinitenge, Jukumu Letu, Zali la Mentali na nyingine nyingi alizofanya na kundi lake la Hard Blasters na hakika haziwezi kukosekana kwenye hii listi.
Ukija kwa Afande, ngoma za Watu Pori, Darubini, Mkuki Moyoni, Ndugu Zangu, Mayowe na nyingine kibao.
Sasa mkumbuke Solo Thang na ngoma zake za Mambo ya Pwani, Mtazamo, Homa ya Dunia na Kilio Changu. Nazo ni vigumu kukosekana kwenye listi hii.
Ukweli ni kwamba ngoma za kale zipo nyingi na kwa mpenzi yeyote wa muziki ni lazima atakuwa na listi yake. Kuna mwingine anaweza kusema mbona sijamuona Fid Q, AY, MwanaFA, Balozi Dolla Soul, Lady Jaydee, Roho 7, Temba na Chegge na makundi mengi kama East Cost, Daz Nundaz, University Corner, Solid Ground Family na mengine mengi, ni kwa sababu ngoma zipo kibao.
Hapa nilikuwa najaribu tu kukukumbusha mpenzi msomaji ngoma chache tu na unaweza kuitumia siku hii ya Alhamisi, kusikiliza ngoma zako nyingine kali za kitambo kushibisha listi yako ya TBT ya Kibabe!
Na.BONIPHACE NGUMIJE
The post Ngoma Hizi ni TBT ya Kibabe appeared first on Global Publishers.