NEWS

1 Aprili 2018

Askofu Malasusa aonya Watanzania kuhusu amani......akemea chuki, visasi

Watanzania wameaswa kuondoa roho za chuki na visasi, badala yake waishi kwa amani kwa sababu wameumbwa kwa mfano wa Mungu.
 
Hayo yamesemwa leo Jumapili Aprili mosi 2018 na Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania ( KKKT),  Alex Malasusa wakati wa adhimisho la ibada ya Pasaka katika Kanisa la Azania Front jijini Dar es Salaam.
 
Dk Malasusa amesema Watanzania wanapaswa kufungua masikio na kusikia agizo la Mungu ili kulinda amani.
 
"Dunia ina mambo mengi, dunia ina kelele nyingi, fungua masikio na usikilize Mungu anakwambia nini na Roho Mtakatifu akikwambia nenda ukashuhudie atakuongoza kufuata yale uliyoyasikia yapate kutendeka katika maisha yako," amesema Dk Malasusa.
 
Amesema binadamu hapaswi kuishi kwa huzuni na manung'uniko, wala kukata tamaa katika maisha yake.
 
"Kuna watu wamezaliwa kuwapelekea wenzao hofu, lakini sisi Wakristo tumezaliwa na kuagizwa kuwaletea watu matumaini na kuhubiri amani," amesema Dk Malasusa.
 
Amesema wasije kutokea watu wakavuruga amani kwa kuwa itakuwa ni vigumu kuirejesha, hivyo Wakristo wanapaswa kusimamia maandiko katika kuhubiri amani na si kusikiliza maneno kutoka sehemu tofauti.
 
"Ndiyo maana tunafuatwa na kuambiwa tuhubiri amani kwa sababu wanaamini dini zina nguvu katika kuhubiri amani na rahisi waumini kuyasikiliza kama ilivyo kwa maandiko," amesema Dk Malasusa.