Ndege ya tatu aina ya Bombardier Dash 8 Q400 itawasili na kupokewa nchini leo Jumatatu Aprili 2,2018 saa 10:00 jioni.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi katika mtandao wa kijamii wa Twitter amesema hayo.
Ndege hiyo pamoja na nyingine mbili zilizopo nchini ni utekelezaji wa mpango wa Serikali katika kulifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
Ndege hiyo awali ilitarajiwa kuwasili nchini Julai mwaka jana ikiwa ni miongoni mwa zingine mbili zenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 70 ambazo zinaendelea kutoa huduma nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi amekaririwa na gazeti la Serikali la Habari Leo akisema ndege hiyo iliondoka Canada tangu Ijumaa Machi 30,2018.
“Tofauti na ndege kubwa zinazoweza kusafiri moja kwa moja, ndege hii italazimika kusimama kwenye vituo kadhaa katika nchi itakazopitia kabla ya kuwasili muda wowote kesho (leo)” alikaririwa Matindi na gazeti hilo.