Kikosi cha timu ya Simba.
PONGEZI zangu za dhati ziende kwa mwekezaji wa Simba, Mohamed Dewji ‘Mo’ kwa kile ambacho alikifanya juzi Jumatatu kwa kutoa tuzo kwa wachezaji na watu mbalimbali wa timu hiyo. Ni jambo ambalo linaamsha hamasa kwa kila mchezaji kwa ajili ya kupambana kuitumikia timu.
Niwapongeze wote ambao wamepata tuzo na hata wale ambao hawajapata basi ni wazi kwamba nao wajitoe ili siku nyingine nao waweze kupata fursa kama hiyo ya kutwaa tuzo. Pia kwa klabu nyingine kufanya kitu kama hicho siyo dhambi kwani kinaongeza upambanaji kutoka kwa mchezaji mmoja kwenda mwingine.
Baada ya hayo, sasa acha niende moja kwa moja kwenye mada yangu husika; wikiendi iliyopita michuano ya SportPesa Super Cup ilihitimishwa kule Kenya. Ikumbukwe kwamba kampuni ya SportPesa ndiyo wadhamini wa klabu zetu za Simba, Yanga, Singida United na JKU kutoka visiwani Zanzibar.
Mwisho wa fainali hiyo ambayo kwa upande wetu Tanzania tuliwakilishwa na Simba, ilimalizika kwa kikosi hicho kuchapwa mabao 2-0. Mabao hayo walifungwa siyo kwa kubahatishwa bali yalitokana kabisa na uwezo wao waliouonyesha kwenye mchezo huo.
Kikosi cha timu ya Yanga.
Licha ya kukosa kitita cha milioni 68 lakini wamekosa nafasi ya kwenda nchini England kucheza na Everton na kuwaruhusu kwa mara nyingine tena Gor Mahia kucheza na timu hiyo kama walivyofanya mwaka jana kwenye ardhi yetu jijini Dar.
Kwangu mimi naona kabisa timu zetu zimevuna kile ambacho walikipanda kabla ya kuanza kwa tuzo hizi; ukitazama jinsi wawakilishi wetu namna walivyoondoka hapa nchini utabaini kabisa kwamba walienda kimasihara na kutoyapa kabisa uzito mashindano haya ambayo kama yangetumika vizuri, nadhani ingekuwa fursa nzuri kwa wachezaji wetu kutoka kisoka.
Wawakilishi wote wanne, Simba, Yanga, Singida United na JKU walikuwa na maandalizi ya kulipua kabla ya kwenda Kenya ambapo walikutana na wenzao ambao wanajua umuhimu wa mashindano hayo na mwisho ndiyo tumejikuta tukiambulia nafasi ya pili na tatu huku tukiiacha kabisa nafasi ya kwenda England kucheza na Everton.
Nasema maandalizi ya kulipua ni kutokana na aina ya matokeo ambayo timu zetu ziliyapata tangu kuanza kwa mashindano hadi pale yanapoisha. Katika dakika zote ambapo wawakilishi wetu walishuka dimbani hakuna hata timu moja ambayo ilionja utamu wa ushindi katika dakika 90 zaidi ya kusubiri faraja ya penalti kwa ajili ya kuwavusha na kuingia hatua zinazokuja.
Nitoe rai kwamba tunatakiwa kubadilika hasa pale inapokuja michuano ya namna hiyo kwa kuhakikisha kwamba tunajiandaa kikamilifu kwa ajili ya kushindana na siyo kushiriki kama walivyofanya walioenda Kenya kuona kwamba licha ya kutwaa kombe lakini tunapata fursa kama hizo za kwenda kucheza nje ya nchi.
Niwapongeze Gor Mahia kwa umakini ambao waliounyesha tangu walipoanza kucheza mechi yao ya kwanza na walikuwa wanajua nini ambacho wanakitafuta ndani na nje ya uwanja na ndiyo maana mwisho wakafanikiwa kutwaa ubingwa.
Kucheza ndai ya Goodson Park ambao ni Uwanja wa Everton kutawapa nafasi wachezaji wa Gor Mahia kuonekana na mawakala wa kimataifa ambao wataweza kuwachukua na kuwapeleka hata katika ligi za madaraja ya chini sitarajii kuona kikosi hicho kikienda England na kurudi bila ya faida yoyote.
Nafasi hiyo ilitakiwa iwe kwa nyota wetu wa hapa nchini lakini imeshindikana kwa sababu tu hawakutulia maanani kombe kama hilo na kupeleka timu ambazo ni dhaifu kuliko wapinzani wao, kitendo kama hicho tusikirudie tena pale itakapotokea michuano kama hiyo.
Makala na Mohammed Hussein

The post Simba, Yanga Zilienda Kiujanja-Ujanja Kenya, Zimestahili Zilichokipata appeared first on Global Publishers.