NEWS

18 Agosti 2018

Katibu Mkuu CCM Dkt. Bashiru Ayachamba "Mataifa ya Magharibi" Kwa Kuingilia Siasa za Mambo ya Ndani Tanzania

Na Is-haka Omar, Zanzibar.
Katibu  Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Dk.Bashiru Ally amezitadharisha baadhi ya nchi za kigeni kuacha tabia ya kuingilia siasa za ndani ya nchi.

Amesema lazima nchi hizo hasa zenye balozi Tanzania ziheshimu Katiba na miongozo ya kisheria ya nchi, vinginevyo Tanzania itashindwa kuvumilia uchochezi unaofanywa na baadhi ya balozi zinazowakilisha nchi hizo Tanzania.
 
Hayo ameyasema leo wakati akizungumza na wananchi na wanachama wa CCM katika viwanja vya  Afisi kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar makuu

Dk. Bashiru amesisitiza kuwa Tanzania ni taifa huru linalojitawala lenyewe na hakuna nchi yoyote itakayoweza kuyumbisha demokrasia ya nchi hiyo.

Amesema kumejitokeza baadhi ya mataifa yanayojifanya viranja wa demokrasia ambayo yamekuwa na tabia ya kutoa matamko ya kuhusu ushindi wa CCM wakati haijasajiliwa kufanya kazi za kisiasa.

Katibu Mkuu huyo ameeleza kuwa katika siku za hivi karibuni kumetokea taifa moja la kibeberu linatuma matamko kwenye mitandao ya kubeza ushindi wa CCM hivyo wanatakiwa waheshimu utawala na demokrasia ilioko nchini.

Dk.Bashiru amefafanua kuwa hakuna taifa lenye haki ya kubeza ushindi wa CCM inaoupata katika chaguzi ndogo zinazofanyika nchni, kwani kufanya hivyo ni kuingilia siasa za ndani za taifa hili.

Katika maelezo yake amebainisha kwamba kinachotakiwa kitambulike ni kuwa CCM haitishwi na matamko ya aina hiyo ya kuibeza

Amesema Tanzania inaendeshwa kwa misingi ya demokrasia ya kweli kwa kupitia misingi ya Azimio la Arusha na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 hivyo waache kuingilia shughuli za uendeshaji wa Tanzania.

Amesema wanaandika matamko ya uongo ya kudanganya ulimwengu ya kuwa Tanzania hakuna uhuru na CCM ina iba kura kwenye uchaguzi na wanatakiwa kutambua CCM imeshinda kutokana na kuwa wananchi wamekuwa na matumaini na CCM katika kutekeleza ilani zake.

Dk.Bashiru ameongeza kwa kusema kuwa  uhuru wowote wa taifa haupatikani ovyo katika kujitawala, hivyo vijana wanatakiwa kuzingatia historia ya ukombozi wa taifa la Tanzania ili kuendeleza kudumisha amani iliyopo.

Aidha alisema, CCM imeamua kulinda rasilimani, mali na utu wake bila ya kuhitaji msaada wa viranja hao wa demokrasia katika utawala wao.

Katibu Mkuu huyo ameeleza kuwa uhuru huu ambao upo wa kujitawala umepiganiwa na hatujapewa kwenye kupitia sahani ama msaada, hivyo aliwataka mataifa hayo makubwa na madogo kupitia balozi zake kuacha kudharau CCM ambayo imekomboa uhuru wa kujitawala.