NEWS

15 Agosti 2018

Kikwete Amjulia Hali Kigwangalla Muhimbili – Pichaz

Rais Mstaafu wa awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akimjulia hali Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Hamisi Kigwangalla kitengo cha mifupa MOI anapopatiwa matibabu. Kulia ni Mke wa Waziri Dk Kigwangalla, Dkt. Bayoum Awadhi Kigwangalla.

 

Rais Mstaafu wa awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete jioni ya tarehe 14, Agosti 2018 amemtembelea na kumjulia hali Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla aliyelazwa katika wodi maalum kitengo cha Taasisi ya mifupa MOI, hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.

 

Rais Mstaafu wa awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na Andrew Chale ambaye ni Mwandishi wa Habari Maalum wa Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Hamisi Kigwangalla. Kulia ni Dkt. Bayoum Awadhi Kigwangalla mke wa Waziri Dkt.Kigwangalla.

 

Hii inakuwa ni mara ya pili kwa Kikwete kumtembelea Dk Kigwangalla ambapo awali alimtembelea Agosti 8, alipokuwa amelazwa Wodi ya Mwaisela akipatiwa Matibabu ya awali. Kikwete amemtakia kila lakheri katika kipindi hiki kwa kuuguza majeraha ya mkono na sehemu za mwili ikiwemo mbavu ambazo kwa sasa hali yake inaendelea kuimarika kwa majibu wa Madaktari wa kitengo hicho cha mifupa MOI.

Awali tokea kufanyiwa operesheni ya mkono ameweza kufanya mazoezi taratibu ikiwemo kutembea mwenyewe katika viunga hivyo vya Muhimbili. Dkt. Kigwangalla alipata ajali ya gari mnamo Agosti 4, 2018 huko Manyara akiwa katika ziara ya kikazi ambapo katika ajali hiyo iliyokuwa na watu 6, watano walijeruhiwa na mmoja alifariki dunia ambaye alikuwa afisa habari mwandamizi wa Wizara hiyo, Hamza Temba.

Na Andrew Chale.

The post Kikwete Amjulia Hali Kigwangalla Muhimbili – Pichaz appeared first on Global Publishers.