WAKATI Jumatano ijayo Ligi Kuu Bara ikitarajiwa kuanza, tayari Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, amesema mshambuliaji wa timu hiyo, Heritier Makambo atafunga mabao 30 na kuwa mfungaji bora.
Mpaka sasa Makambo ameichezea Yanga mechi mbili za kirafiki wakiwa mkoani Morogoro na amefunga mabao mawili.
Kutokana na hali hiyo, Zahera amewataka mabeki wa ligi kuu watakaokuwa wakikutana na Makambo wajiandae kukabiliana na mziki wa mshambuliaji huyo ambaye kiwango chake kimekuwa kikiongezeka kila siku.
Zahera ameliambia Championi Jumamosi kuwa, licha ya Makambo kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kabla ya kujiunga na Yanga, sasa amekuwa akimpa mazoezi makali ambayo yanamfanya awe fiti, hali inayomfanya aseme mchezaji wake huyo atafunga mabao 30 na kuwa mfungaji bora.
“Maendeleo ya Makambo siyo mabaya, anaendelea vizuri na kiwango chake kinaongezeka kila siku. Atakuwa na msaada mkubwa sana katika kikosi changu na tayari ameonyesha kuelewana vilivyo na Mrisho Ngassa, kwa hiyo mabeki wajipange kwelikweli.
“Kwa namna ninavyomfahamu na nimuonavyo hapa mazoezini ninaamini anaweza kufunga mabao 30 peke yake kama hatapata majeraha, kwa hiyo naamini pia anaweza kuwa mfungaji bora, subiri ligi ikianza mtaona makali yake,” alisema Zahera.
Naye Makambo amesema kuwa yupo tayari kuipigania timu yake lakini ameomba apewe mechi nne tu kwani kwa sasa mwili wake haupo fiti, baada ya hapo ataanza kuonyesha makali yake.
“Naendelea vizuri, namshukuru Mungu na sasa nipo fiti ila ili niweze kuwa sawa kabisa nahitaji mechi tatu au nne hivi kwani mwili sasa ni kama umechacha kutokana na mazoezi magumu niliyokuwa nafanya kwa ajili ya kuwa fiti.
“Baada ya hapo naamini nitakuwa katika kiwango changu ambacho nakijua mwenyewe, tofauti na cha sasa.”
The post Kocha Yanga Ampa Makambo Mabao 30 appeared first on Global Publishers.