BAADA ya taarifa kusema Obrey Chirwa anaweza kurejea kikosini humo, ghafla Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema hamtaki lakini sasa ameonekana kulainika na kukubali staa huyo arejee, hiyo ni baada ya kufanyika kwa kikao cha dharura.
Chirwa ambaye alidumu kwa misimu miwili Yanga, aliwahi kuripotiwa kugoma kuichezea timu hiyo akishinikiza alipwe fedha zake wakati huo Yanga ilikuwa kwenye hali mbaya kiuchumi jambo ambalo lilimfanya Zahera aseme hatakuja kufanya kazi na mshambuliaji huyo.
Baada ya kumaliza mkataba na Yanga, Chirwa aliondoka na kwenda kujiunga na Klabu ya Nogotoom ya nchini Misri, na huko pia inadaiwa amevunja mkataba kutokana na kushindwa kumlipa stahiki zake kimkataba na hivi karibuni alikuwepo Uwanja wa Taifa kuishuhudia Yanga ikicheza na Alliance.
Chanzo makini kimeliambia Championi Jumamosi kuwa, baada ya sekeseke hilo la Zahera kukaza Chirwa kurudi Yanga kutokana na ishu ya kinidhamu, viongozi wa timu hiyo walilazimika haraka kufanya naye kikao cha dharura ambacho kilifanyika kwa siku mbili wakimtaka akubali mshambuliaji huyo asajiliwe.
Chanzo hicho kimesema kulikuwa na mvutano mkubwa baina ya viongozi wa kamati na kocha Zahera ambaye baadaye alikubali na kuwapa sharti kwamba ni lazima Chirwa amuombe radhi kwa yale aliyoyafanya kwa kocha kabla ya kuondoka.
“Suala la Chirwa kurudi Yanga linaonekana kuwa mada kubwa kwa uongozi wetu hasa kupitia kamati za usajili na ile ya mashindano ambapo wamefuata masharti ili wamrejeshe Chirwa lakini wakawa wanakwama kutokana na msimamo wa kocha Zahera kutomuhitaji Chirwa.
“Mvutano huo umesababisha waitishe kikao cha dharura ambacho kilichukua siku mbili, cha kwanza walifanya wenyewe bila kocha na siku iliyofuata wakamjumuisha Zahera ambaye walimuomba amsamehe Chirwa ili waweze kumsajili dirisha dogo jambo ambalo ameonekana kuelekea kukubaliana nalo.
“Lakini alitoa masharti yake kwa wajumbe hao kwamba Chirwa mwenyewe kuitwa kwenye kikao ili aombe radhi kwa yale aliyoyafanya kwa kocha kabla ya kuondoka na pia kamati hiyo kuhakikisha inasimamia nidhamu yake endapo atarejea,” kilisema chanzo hicho.
Zahera alisema: “Hakuna viongozi wengine niliokutana nao zaidi ya Hussein Nyika (Mwenyekiti Kamati ya Usajili) na Mustafa Olungu (makamu) na kuzungumza nao kuhusiana na suala la Chirwa kikubwa walinipongeza kwa msimamo wa kutomkubali Chirwa kurejea Yanga, nilichukizwa na kitendo cha mtu kutoka ndani ya timu ambaye alimtumia tiketi Chirwa ili aje nchini kujiunga na Yanga bila mimi kujua.
“Baada ya Chirwa kufika kuna mtu alianza kuwashawishi Nyika na Olungu wakubali kwa pamoja ili wamrudishe ndani ya kikosi cha Yanga kabla hilo halijafanikiwa wakasikia kauli yangu kuwa simtaki Chirwa kutokana na matatizo mengi aliyoifanyia timu kabla ya kuacha na sisi. Mimi ni kama kocha nilisema hivyo kwa kuwa sikuwa najua na Nyika na Olungu walinifafanulia vizuri kwa hiyo sasa nimenyamaza na kuwasikiliza watakachoafikiana wao nipo tayari.”
Musa Mateja, Dar es Salaam
The post ISHU YA CHIRWA, ZAHERA AKUBALI YAISHE appeared first on Global Publishers.