Jalada la kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili, aliyekuwa Kamishana wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake wawili, linafanyiwa kazi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi amedai leo Ijumaa Oktoba 26, 2018, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Huruma Shahidi wakati kesi hiyo ilipotajwa.
Kishenyi amedai kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba Takukuru wapo katika ukamilishaji wa uchunguzi ili kesi hiyo iweze kuendelea na hatua nyingine.
"Upelelezi bado haujakamilika na vyombo vinavyofanya uchunguzi vipo katika hatua ya ukamilishaji uchunguzi hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kuangalia kama vyombo hivyo vya uchunguzi vimeshakamilika uchunguzi," amedai.
Kishenyi baada ya kueleza hayo, wakili wa utetezi, Oscar Magolosa, alieleza kuwa ni rai yao kuwa upelelezi wa shauri hilo utakamilika haraka ili kesi hiyo iweze kuendelea.
"Ni matumaini yetu upelelezi wa kesi hii utakamilika kwa wakati kama ambavyo, upande wa mashtaka ulivyoiambia Mahakama hapa kuwa vyombo vya uchunguzi vinakamilisha uchunguzi wao," amedai Magolosa.
Baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote, Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 9, 2018 kesi itakapotajwa tena.
Pamoja na Kitilya ambaye ni mwenyekiti wa Kampuni ya Uwekezaji wa Mitaji na Dhamana (Egma), washtakiwa wengine ni waliokuwa maofisa wa Benki ya Stanbic, Shose Sinare na Sioi Solomon.
Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha.
Washtakiwa hao wanaendelea kusota rumande kwa takribani miaka mitatu sasa kutoka na upelelezi wa kesi hiyo kudaiwa kuwa haujakamilika.