
ZAIDI watu 50 wamepoteza maisha kutokana na maporoko ya ardhi na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa inayoendelea kunyesha mashariki mwa Uganda. Mamia ya watu bado hawajulikani walipo huku maofisa katika wilaya ya Bududa wakihofu kuwa idadi ya waliopoteza maisha huenda ikaongezeka. Walioshuhudia mkasa huo wanasema kuwa mwamba ulidondoka mtoni na kupasua kingo za mto hali iliyosababisha maji yaliyochanganyikana na matope kuanza kusomba watu vijijini.
Serikali imesema vikosi vya uokoaji vimepelekwa katika eneo hilo karibu na mpaka wa Uganda na Kenya lakini miundo mbinu ya barabara na daraja iliyoharibiwa imekwamisha shughuli za uokozi. Picha kutoka eneo la tukio zinaonyesha watu wakitoa miili kutoka ndani ya tope na kuiweka kando. Maporomoko mengine ya udongo yaliyoshuhudiwa katika eneo hilo la Bududa yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 300 mwaka 2010.

Mwanahabari wa kujitegemea, Shwahib Ibrahim, ameliambia shirika la utangazaji la Uingereza (BBC) kuwa baadhi ya wakazi mpaka sasa hawajui wapendwa wao wako wapi. Ibrahim pia amesema shirika la Msalaba Mwekundu limekuwa likiwasaidia waathirika wa mkasa huo tangu jana.
Kwa upande wake, msemaji wa shirika la Msalaba Mwekundu, Irene Nakasiita, amesema maji yalipoanza kuteremka, yalibeba mawe makubwa ambayo yaliharibu nyumba za watu.
Kufuatia ttukio la mwaka 2010, wakazi wa sehemu hiyo waliiamriwa kuhama eneo hilo lakini wengi wao walirejea kwa kuvutiwa na ardhi yenye rutuba na upendo wa makazi yao ya asili.
The post Maporomoko ya ardhi yawaua zaidi ya 50 Uganda appeared first on Global Publishers.