Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mwibara, Bunda mkoani Mara, Betha Sayi, ameingia matatani baada ya kudaiwa kuwadhalilisha wanafunzi wa kike wa shule hiyo.
Sayi anatuhumiwa kuwavua nguo zote wanafunzi hao, zikiwamo za ndani na kuwashika shika katika sehemu za siri kwa madai kuwa anawapima kama wana ujauzito
Tuhuma hizo zilitolewa jana na wanafunzi hao, hali ambayo ilisababisha taharuki kwa wazazi ambao walisema hawawezi kuvumilia kitendo hicho cha udhalilishaji, ukatili wa kijinsia na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Ilidaiwa kuwa, mwalimu huyo alifika shuleni hapo juzi asubuhi na kuwaita wanafunzi hao kila mmoja katika ofisi yake na kuanza kuwavua nguo zote na kisha kuwafanyia kitendo hicho cha udhalilishaji.
Aidha, imeelezwa kuwa, baada ya kuwavua nguo zote na kuwafanyia udhalilishaji huo, alichukua nguo zao za ndani za wanafunzi hao na kuziweka ndani ya boksi.
Hali hiyo iliwafanya baadhi ya wanafunzi hao kukimbilia nyumbani kwao na kutoa taarifa kwa wazazi wao, ambao walitahamaki na kwenda shuleni hapo na kisha wakatoa taarifa katika kituo kidogo cha polisi Kibara.
Akizungumzia sakata hilo, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mwibara, Sylivanus Manyapara, ambaye pia ni Kaimu Mratibu Elimu Kata, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kwamba mwalimu huyo alipelekwa katika kituo cha polisi Kibara, akiwa na nguo za ndani za wanafunzi hao zilizokuwa kwenye boksi.
Mnyapala alisema tayari tukio hilo limeripotiwa katika kituo kidogo cha polisi Kibara na mwalimu huyo alishikiliwa kwa muda kisha akapewa dhamana na nguo hizo ziko kituoni hapo kama kielelezo.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kibara B, Mafwili Mnyanga, alisema kitendo hicho kimelaaniwa na wazazi na wananchi wa kijiji hicho.
"Kitendo hiki ni kibaya sana na kinaweza hata kusababisha vurugu kwani watoto kufanyiwa hivyo ni unyama. Wamefanyiwa ukatili mkubwa na pia huo ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu kwa hiyo sisi wazazi pia tumeathirika kwa kitendo hicho," alisema kwa njia ya simu.