
Kocha Mkuu wa Lipuli FC ya Iringa, Selemani Matola.
KOCHA Mkuu wa Lipuli FC ya Iringa, Selemani Matola, amesema kuwa, kutokana na hali ngumu ambayo inazikabili klabu za ligi kuu hivi sasa, kuna uwezekano mkubwa wa kushindwa kuendelea mzunguko wa pili.
Mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara unatarajiwa kufikia tamati hivi karibuni baada ya timu zote 20 kucheza mechi 19 ambapo ligi hiyo inachezwa bila ya kuwa na mdhamini kutokana na ukata ambao ulijitokeza.
Akizungumza na Championi Jumatano, Matola alisema kuwa, jinsi ligi inavyozidi kusonga mbele ndipo inapozidi kuwa mbaya zaidi, kutokana na ukata wa kila timu unaozikabili kwa wachezaji kadhaa kudai mishahara hivyo inakatisha tamaa.
“Mzunguko wa pili utakuwa mgumu sana kwa kuwa hali ni mbaya kwa kila timu, wachezaji wamekuwa wakidai mishahara, inakatisha tamaa wachezaji wamekuwa wakicheza ligi bila ya kuwa na posho wala mishahara, nadhani kuna timu ambazo zitashindwa kumaliza ligi, hilo lipo wazi kabisa.
“Watu wametumia nguvu sana katika mzunguko wa kwanza sasa wameishiwa pumzi hawana fedha hivyo kuna uwezekano mkubwa hali ikawa mbaya zaidi mzunguko wa pili.
“Fedha za Vodacom zilikuwa zikitusaidia sana lakini kutokuwepo kwa fedha hizo sasa mambo yanazidi kuwa magumu na ligi haiwezi kuwa na ubora,” alisema Matola.
The post Matola: Kuna Timu Hazitamaliza Ligi appeared first on Global Publishers.