NEWS

3 Aprili 2019

DAKTARI NUSURA AUE MTOTO!

MTU akiitwa daktari maana yake ni: “Mtaalamu aliyepata shahada ya juu kabisa; mganga aliyehitimu katika elimu ya tiba ya dawa za kisasa, (Tabibu).” 

 

Ukisikia daktari nusura auwe mtoto lazima utajiuliza; kulikoni tabibu aache kazi ya kutibu kisasa na kujikuta katika skendo hiyo nzito?

 

Ijumaa Wikienda lina kisa kizito kilichojaa tuhuma dhidi ya daktari mmoja anayedaiwa kutaka kusababisha kifo cha mtoto Wema Ally mwenye miezi sita mkazi wa Magomeni jijini Dar. Kwa kuzingatia muongozo wa kitaaluma, jina la daktari na hospitali anayofanyia kazi litahifadhiwa kwa sasa na kwamba kitakachoripotiwa leo ni simulizi ya tukio la kusikitisha lililompata mtoto huyo.

 

KARIBU KWA SIMULIZI

Akizungumza hivi karibuni na Ijumaa Wikienda baba mzazi wa mtoto huyo aitwaye Ally Herry, mkazi wa Magomeni alisema Februari 22, mwaka huu mwanaye aliugua na kulazimika kumpeleka hospitali kwa ajili ya matibabu.

 

“Mtoto wangu alikuwa anatapika na kuharisha, mimi na mke wangu tulimchukua na kumpeleka Zahanati ya Mzimuni ambapo nashukuru Mungu walitupokea vizuri na mtoto akatibiwa. “Tulirudi nyumbani, lakini Machi 7, hali ya mtoto ilibadilika ikabidi turudi palepale Mzimuni. “Lakini kutokana na udogo wa Zahanati, madaktari walitupa rufaa ya kwenda (jina la hospitali linahifadhiwa),” alisema baba wa mtoto huyo.

 

Aliongeza kuwa, Machi 9 walifika katika hospitali hiyo na kupokelewa kisha kukutana na daktari ambaye alipomtazama mtoto Wema akasema ana maambukizi kwenye njia ya haja ndogo ‘UTI’ na malaria. Baada ya kupewa majibu hayo daktari huyo aliwaandikia shindano 10, tano za kutibu malaria na tano za kutibu UTI sambamba na dawa mseto ambazo walikwenda kuchukua kwenye dirisha kunakotolewa dawa.

WEMA AZIDI KUZIDIWA

Baba wa mtoto huyo analiambia Ijumaa Wikienda kuwa pamoja na kutumia dawa hizo kama walivyoshauriwa na daktari, Wema hakupa nafuu. “Tulipoona mtoto anazidi kudhoofika Machi 14 ikabidi tumrudishe tena hospitalini hapo ili akachekiwe zaidi kwa sababu mimi nilipomuona nilihisi amepungukiwa maji mwilini,” alisema.

 

HUYU HAPA TABIBU WA WATOTO

Pengine kwa kuzingatia neno halisi la daktari, baba wa Wema akiwa na mkewe walielekezwa kwenda kumuona daktari ambaye amebobea kutibu watoto. Baba huyo anaeleza kuwa walipomuona daktari huyo walimweleza hali ya mtoto kuwa analegea na kwamba yuko kwenye hali mbaya wakiamini kuwa hatua ya uchukuaji vipimo ingefanyika lakini haikuwa hivyo.

 

DAKTARI AWAANDIKIA DAWA

Katika hali hiyohiyo ya kutokupimwa na kuelezwa kinagaubaga tatizo linalomsumbua Wema, daktari huyo anadaiwa kuwa aliinama na kuwaandikia dawa aina ya Ciprofloxacin na Oro na kuwataka waende dirishani wakachukue.

 

MTOA DAWA AMSHANGAA DAKTARI

Inaelezwa kwamba baada ya wazazi wa Wema huku wakiwa na mtoto wao mgonjwa kufika kwenye dirisha la kuchukulia dawa mtoa dawa alipigwa na butwaa na kuanza kuwauliza:

 

MTOA DAWA: Hizi dawa anaenda kunywa nani?

BABA: Mwanangu.

MTOA DAWA: Ana umri gani?

BABA: Miezi sita.

 

MTOA DAWA: Nani kakuandikia?

BABA: Kwani vipi mbona maswali mengi?

MTOA DAWA: Kama ni kwa matumizi ya huyo mtoto mimi siwezi kutoa dawa hizi, rudi kwa daktari ukamuulize vizuri.

BABA: Nirudi kwa daktari tena?

 

MTOA DAWA: Ndiyo na ikiwezekana njoo naye hapa.

Baada ya kuambiwa hivyo Ally alifura kwa hasira huku imani yake ikiwa kwa ‘daktari’ kwamba hawezi kuwa na kosa katika kutoa tiba.

Ally alisema alilazimika kuondoka kwenye dirisha hilo kwa hasira na kurejea kwa daktari wake kama mtu anayesema; “Sipendi usumbufu.” Ingawa hakufafanua lugha aliyotumia kumwambia daktari kwamba amegomewa na mtoa dawa kupewa huduma ila unaweza kuhisi alisema:

 

“Dokta huyo nesi mimi simwelewi amegoma kutoa dawa anasema eti nije nikuulize vizuri na ikiwezekana twende wote kwake, hivi anajitambua kweli au anataka rushwa? Ally anasema alipomweleza daktari kuwa mtoa dawa ametilia mashaka dozi hiyo, mganga huyo alimwambia: “Kwa nini amegoma? Mwambie akupe.”

 

WAPEWA DAWA

Kwa kuwa ushauri wa mtoa dawa haukuzingatia na kwamba daktari aligoma kwenda kumsikiliza akaona isiwe shida akalazimika kuwapa dawa hizo.

“Nilienda kumpa ile dozi mtoto wangu lakini cha kushangaza, alipokaribia kumaliza dozi hali yake ilibadilika akaanza kuvimba mwili. “Kupumua kwake kukawa kwa shida, tumbo lake likiwa limejaa maji, tulichanganyikiwa, tarehe 20/03/2019 ikabidi turudi pale hospitali. “Tulimkuta daktari mwingine wa kike, ambapo baada ya kumuangalia mtoto akasema hali yake ni mbaya.

 

“Akasema mtoto apelekwe haraka maabara na akitoka huko apelekwe Hospitali ya Mwananyamala kwa ajili ya vipimo zaidi. “Tulienda maabara na baada ya hapo moja kwa moja tukaenda Mwananyamala, tulipokelewa vizuri ambapo tuliambiwa mtoto amepungukiwa damu. Baadaye mtoto akalazwa kwa siku tatu.

 

WAHAMISHWA HOSPITALI

Ally anaeleza kwamba, baada ya kupatiwa matibabu madaktari walitushauri tumpeleke mtoto Hospitali ya Mloganzila ili afanyiwe uchunguzi zaidi. “Pale pia tulipokelewa vizuri sana na madaktari, mtoto akapimwa na kugundulika kuwa figo moja ilikuwa imefeli kutokana na kuwepo kwa sumu nyingi mwilini.

 

Majibu hayo ya sumu yalizidi kuwachanganya wazazi wa mtoto huyo na kwamba alipowadodosa zaidi baadhi ya madaktari walisema imechangiwa kwa kiasi kikubwa cha dozi ya Cipro aliyopewa jambo ambalo lilimfanya Ally akumbuke mgomo wa kupewa dawa aliopewa na yule nesi.

 

HALI YA WEMA YAZIDI KUWA TETE

Pamoja na tiba nzuri zilizotolewa na madaktari wa hospitali hiyo ya Mloganzila kujaribu kuokoa maisha ya Wema bado hali yake ni tete kutokana na ukweli kwamba njia za utoaji sumu mwilini ni ngumu.

 

“Ililazimika kutoboa tumbo, ili kumuwezesha kutoa uchafu lakini mahali alipotobolewa hapajafunga na kwamba pamevimba sana,” alisema baba huyo wa Wema. Kwa mujibu wake madaktari hivi sasa wamelazimika kuachana na njia ya kutoa uchafu kupitia tumboni na badala yake wanatumia njia ya kuingiza mipira kwenye njia ya haja ndogo jambo ambalo limekuwa zito kutokana na njia ya mtoto kuwa nyembamba.

 

BABA AOMBA MSAADA

Kufuatia mkasa mzito wa mtoto wake baba yake mzazi ameiomba serikali kuingilia kati huku akiwatolea mwito Watanzania wenzake kumsadia kwa hali na mali ili kuweza kuokoa maisha ya mwanaye. “Hapa nilipo sina fedha za kuweza kumtibu mwanangu, changamoto ni nyingi mno katika kumuuguza nawaomba wasamaria wema watusaidie chochote tuokoe maisha ya mtoto wetu mpendwa,” alisema baba huyo.

 

HOSPITALI YATOA KAULI; YASIKITIKA

Kutokana na kadhia hiyo baba wa Wema akiongozana na mwandishi wetu walilazimika kufika kwenye hospitali hiyo kwa lengo la kupata maelezo ya kina kuhusu tuhuma za daktari wao kuchangia matatizo ya mtoto ambapo mmoja wa madaktari viongozi alisema suala hilo wanalishughulikia.

 

“Hili suala tumelipokea na kwa kuwa limeshafika kwangu basi ondoeni shaka nitalishughukia kikamilifu. “Ninachowaomba ni kwamba msininukuu kauli zangu kwa sababu mimi si msemaji wa hospitali, nitakachokifanya nitaandika ripoti na kuipeleka kwa wakubwa nao watatoa tamko,” alisema daktari huyo ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.

 

Aidha, daktari mwingine kiongozi alionesha kusikitishwa kwake na tiba hiyo na kuomba atoe fotokopi ya daftari la matibabu ya mtoto huyo ili aweze kuliambatanisha na ripoti ya tuhuma itakayopelekwa kwa wakubwa. Gazeti hili linaendelea kufuatilia sakata hili na kwamba ripoti ambayo imetajwa kutoka Jumatano wiki hii ikipatikana habari zake zitawekwa kwenye gazeti lolote la Global Publishers.

Stori: Hamida Hassan na Memorise Richard ,Ijumaa Wikienda

The post DAKTARI NUSURA AUE MTOTO! appeared first on Global Publishers.