SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, ameiagiza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kumhoji Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, kuhusu uamuzi wake wa kuunga mkono kauli iliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Prof. Mussa Assad kuwa bunge ni dhaifu, na wakati huohuo ameanika hadharani madeni ya mbunge huyo.
Akizungumza baada ya kipindi cha maswali na majibu bungeni leo, Ndugai ametaka kamati hiyo ikutane leo saa 8.00 mchana na kwamba ikiwezekana suala hilo kesho likamilike.
Akisisitiza kwamba haogopi kitu, Ndugai alisema: “Wanaofikiri sisi ni dhaifu, sisi sio dhaifu nishasema nikarudia na narudia tena, yeyote ambaye anaingia katika 18 yangu (eneo la madaraka yake) sisi tuko tayari na yeye.
“Mheshimiwa Lema atakwenda huko na kesho kunako majaliwa tutaifahamu hatma yake. Na mwingine anayejiona anaalikwa kabisa. Nataka sasa tuthibitishe kuwa Bunge hili la kumi na moja kweli lina uongozi na tutathibitisha hatumuogopi yeyote.”
Katika hatua nyingine, Ndugai amemfukuza bugeni, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko (Chadema) baada ya kupiga kelele kumpinga kiongozi huyo wakati akilitaja deni la Lema.
Ndugai alilitaja deni ambalo alisema Lema anadaiwa kutokana na mkopo, hatua ambayo Matiko aliipinga na hivyo kusababisha kuchukuliwa kwa hatua hiyo.
The post SPIKA NDUGAI ATAJA DENI LA LEMA, AMTOA NJE ESTHER MATIKO appeared first on Global Publishers.