NEWS

30 Mei 2019

Bulaya Amhoji Waziri Kutobomoa Nyumba ya Kigogo

Bulaya amhoji Waziri kutobomoa nyumba ya kigogo
Mbunge wa Bunda Esther Bulaya amehoji juu ya kutobomolewa kwa nyumba ya kigogo mmoja wa Kinondoni jijini Dar es salaam bila kutaja jina la mtu huyo kwa kile allichokidai zoezi hilo lilipaswa kutekelezwa muda mrefu lakini halijafanyika.


Esther Bulaya ametoa kauli hiyo Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akiuliza swali kwa Waziri wa Ardhi William Lukuvi, kuhusiana na wananchi wanaojenga kwenye ya mikondo ya maji.

"Serikali imebomoa nyumba zilizojengwa kwenye mikondo ya mito, umebomoa nyumba nyingi Kawe, kuna nyumba ya kigogo imeachwa, lini itavunjwa?", ameuliza Bulaya.

Akijibu swali hilo Waziri Lukuvi amesema suala la ubomoaji wa nyumba Wizara inapokea orodha kutoka kwa Afisa Ujenzi wa Wilaya wao ni watekelezaji tu.

"Oda ya kubomoa inatolewa na Afisa Ujenzi Wilaya, mazoezi haya yamefanyika wilayani Kinondoni, bonde la Msimbazi naomba wananchi wasijenge bila vibali", amejibu Waziri Lukuvi.

Kwa sasa Bunge linaendelea jijini Dodoma ambapo Mawaziri mbalimbali wameendelea kuwasilisha makadirio ya bajeti kwa Wizara zao kwa mwaka wa fedha 2018/2019.