NEWS

30 Mei 2019

POLISI WAANIKA MAPYA WIZI KWA MENGI NYUMBANI

DAR ES SALAAM: Zikiwa zimepita takribani wiki mbili tangu watu wasiofahamika kudaiwa kuingia nyumbani kwa aliyekuwa mfanyabiashara na Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, marehemu Dk Reginald Abraham Mengi, Machame Moshi mkoani Kilimanjaro na kuiba, polisi wameanika mapya kuhusiana na madai hayo. Risasi linakupa full stori. 

 

Siku mbili baada ya kuzikwa kwa mfanyabiashara huyo, zilisambaa taarifa kuwa wezi wameingia katika nyumba yake iliyoko Machame mkoani Kilimanjaro na kuiba vifaa vya thamani na fedha taslimu. Ilielezwa kuwa, vitu vilivyodaiwa kuibiwa ni pamoja na mikufu ya dhahabu, kompyuta mpakato ‘laptop’ pamoja na fedha taslimu ambazo zilielezwa kufika mamilioni.

 

Baada ya kimya kirefu gazeti hili lilimtafuta Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, ACP Hamisi Issah. Katika mahojiano maalum ya moja kwa moja kwa njia ya simu kati ya Risasi Mchanganyiko na kamanda huyo wa polisi, ACP Issah alianika mapya kuhusiana na wizi huo.

 

Mahojiano hayo yalikuwa kama ifuatavyo:

Risasi: Habari yako Kamanda, mimi ni mwandishi wa habari wa Global Publishers.

Kamanda: Salama; nikusaidie nini?

 

Risasi: Kamanda kuna taarifa ziliwahi kutoka kuwa kuna watu wasiojulikana waliingia katika nyumba ya aliyekuwa mfanyabiashara Dk Mengi na kuchukua vitu vya thamani, umeishia wapi upelelezi wa jambo hilo?

Kamanda: Wale vijana bado tunawashikilia lakini siyo kusema ni wezi bali ni watu waliokuwepo msibani lakini waliingia kwenye eneo ambalo hawakupaswa kuingia zaidi ya ndugu na ndiyo sababu hasa ya kuwashikilia.

Siku hiyo kila mtu alisema yeye ni mwanafamilia na kila mtu aliingia mahali ambako hahusiki na matokeo yake ndiyo hayo.

POLISI WAHENYEKA

Risasi: Lakini kamanda, ilidaiwa na kutangazwa kuwa waliiba mikufu, vito vya thamani na mamilioni ya shilingi, hii imekaaje?

Kamanda: Huo ni upotoshaji kabisa, hakuna wizi mkubwa ambao ulitokea zaidi ya kuibiwa vitu ambavyo havifiki hata shilingi milioni moja.

 

Risasi: Ni vitu gani ambavyo mmebaini vilivyoibiwa nyumbani kwa Mengi kamanda?

Kamanda: Vichache tu hata shilingi milioni moja haijafika, muombolezaji mmoja aliibiwa laptop yenye thamani ya shilingi 800,000 za Kitanzania, mtu mwingine aliibiwa shilingi 20,000 na mwingine shilingi 30,000, utaona hapo hata shilingi milioni moja haijafika.

 

Risasi: Kuhusu vito vya thamani na mikufu je?

Kamanda: Ni uzushi na ndiyo maana wanaosema hivyo wanafanya kazi hii iwe ngumu. Tunahenyeka kweli kwa kuwa hakuna ukweli, unaposema mamilioni ya fedha yaliibwa wakati hata milioni haijafika inakuwa kazi ngumu kweli kwetu.

Risasi: Nakushukuru kamanda kwa ushirikiano wako.

Kamanda: Nakushukuru na wewe pia, karibu tena.

 

TUJIKUMBUSHE

Wakati msiba huo mzito ukiombolezwa ilidaiwa kuwa kulikuwa na watu ambao walifaidika kiharamu na msiba huo; kwa kuiba vito, vifaa vya thamani na fedha taslimu katika nyumba mbili tofauti za marehemu Dk. Mengi.

Ilidaiwa kuwa vitu hivyo ni mikufu ya dhahabu, kompyuta mpakato pamoja na mamilioni ya fedha taslimu ambazo kiwango chake hakikuelezwa na ikadaiwa ni mali ya familia na waombolezaji. Dk. Mengi, ambaye pia alikuwa akijihusisha na uchimbaji madini na kumiliki vyombo vya habari, alifariki Mei 2 akiwa Dubai, Falme za Kiarabu na alizikwa kijijini kwao Nkuu, Machame mkoani Kilimanjaro.

 

Msemaji wa familia hiyo, Benson Mengi baada ya tukio hilo alihojiwa akasema hawakuwa tayari kuzungumzia jambo hilo kwa kuwa bado uchunguzi wa polisi unaendelea. “Bado uchunguzi wa polisi unaendelea,” alisema Benson ambaye ni mtoto wa mdogo wake Dk. Mengi anayeitwa Benjamin Mengi. Naye Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Issah alihojiwa kuhusiana na madai hayo akasema tayari wanawashikilia watu wawili wakiwatuhumu kuhusika na wizi huo.

Katika kipindi hicho, Kamanda Issah alisema tukio hilo lilifanywa na watu wanaodaiwa kuwa wa ndani na familia hiyo na taarifa zilionyesha walitokea jijini Dar es Salaam. “Ni kweli nyumbani kwa Mengi kumeibiwa,” alisema kamanda huyo akaongeza, “Suala hilo ni la ndani na tukianza kulishughulikia kikamilifu litahusisha watu ambao ni wa ndani. Sasa sijui tutakuwa kwenye msiba au tutakuwa tunakamatana, maana tumeongeza huzuni juu ya huzuni.

 

“Kumetokea watu mchanganyiko. Familia ile watu wengi walikuwa hawafahamiani, matokeo yake kila mtu anasema mimi na kila mtu anaingia mahali ambako hahusiki na matokeo yake ni wizi.” Alisema tayari polisi inamshikilia mwanamume na mwanamke mmoja ambao wanaonekana ni wageni wa familia hiyo.

 

“Ila bado tunaendelea na uchunguzi, ili kubaini undani zaidi wa tukio hili na kuwapata wahusika,” alisema. Alisema baadhi ya watu ambao hawakutaka majina yao yatajwe, walidai baadhi ya waliohusika walikuwa wamevalia vitambulisho vilivyoandikwa IPP.

 

Dk.Mengi, 77, alikuwa anajihusisha na umiliki wa viwanda kama vya vinywaji baridi, vituo vya televisheni, magazeti na mitandao ya kijamii, na aliwahi kuongoza taasisi mbalimbali za kibiashara na masuala ya kijamii. Baada ya kifo cha mfanyabiashara huyo watu wengi walifika nyumbani kwake jijini Dar es Salaam na Machame, Kilimanjaro kwa ajili ya mazishi na maombolezo.

The post POLISI WAANIKA MAPYA WIZI KWA MENGI NYUMBANI appeared first on Global Publishers.