Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imepokea mashine ya Echo kutoka katika Taasisi ya Save a Child’s Heart kutoka Canada kwa ajili ya kusaidia tiba ya magonjwa ya moyo kwa watoto. Akizungumza na Global Publishers baada ya kupokea mashine hiyo jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Prof Mohammed Janabi alisema kuwa anashukuru sana kwa kupatiwa mashine hiyo ambayo ina uwezo wa kusaidia na kutibu watoto wengi hapa nchini.
“Nawashukuru sana Save a Child’s Heart kutoka Canada kwa mashine waliyotupatia nimepokea kwa furaha kwa kuwa mashine hii ina msaada mkubwa sana kwa watoto wetu wenye matatizo ya moyo na uzuri ni mashine ambayo inahamishika kutoka sehemu moja kwenda nyingine, ina uwezo wa kwenda hadi mikoani kutibu watoto wenye matatizo hayo,” alisema Prof Janabi.
Aidha, Prof Janabi aliongeza kwa kusema kuwa, Tanzania ina mtaalam mmoja mbobezi wa masuala ya upasuaji wa moyo kwa watoto ambaye ni Dr Godwin akisaidiwa na baadhi ya watalaam wasaidizi ambao kwa pamoja wameweza kuwafanyia upasuaji watoto 260.
The post TAASISI YA CANADA YAIPA JKCI MASHINE YA MAGONJWA YA MOYO KWA WATOTO! appeared first on Global Publishers.