NEWS

31 Mei 2019

Waziri Jafo atoa maelekezo maalumu kwa Ma-RC, Ma DC na Wakurugenzi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mh. Suleiman Jafo amewaagiza wakuu wa Mikoa minne iliyopo kwenye mradi wa “lishe Endelevu” kuhakikisha kuwa mikataba hiyo ya utekelezaji wa afua za lishe inawashukie wakuu wa Wilaya, nao wasainiane na wakurugenzi wa halmashauri, nao pia waishushe kwa watendaji wa kata na watendaji hao  wasainiane na watendjai wa vijiji na mitaa ili utekelezaji wa mikataba hiyo kuwa shirikishi bila ya kubagua eneo lolote la utawala.

Amesema kuwa pamoja na utekelezaji wa mradi huo, Waziri wa nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa niaba ya Makamu wa Rais alisainishana mkataba wa utekelezaji wa afua za lishe na wakuu wa Mikoa yote nchini ili kuchochea utekelezaji wa shughuli za lishe hapa nchini, mkataba ambao una viashiria kumi ambavyo vinampima Mkuu wa Mkoa kila baada ya miezi sita na utadumu kwa kipini cha miaka minne kuanzia januari 2018 hadi 2021

“Kwa vile eneo hili ni eneo la mradi maalum, nitatamani sana niweze kuona katika mbao za vijiji vyetu ambavyo miradi hii inatekelezeka, tuwe na taarifa licha ya taarifa ya mapato na matumizi, kuwe na taarifa ambayo inasema katika Kijiji X, Kijiji cha Milepa, Kijiji cha Wampembe ama Kijiji kingine inaonesha watoto wenye udumavu ni wangapi na watoto wenye upungufu wa damu ni wangapi, hili jambo ninlazima tushikane kila mtu atomize wajibu wake kuhakikisha ajenda ya lishe tunaisimamia kwa nguvu zote,” Alisisitiza.

Ameyasema hayo alipokuwa akizindua mradi wa Lishe Endelevu unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Watu wa Marekani (USAID) unaotekelezwa katika Mikoa minne ya Iringa, Dodoma, Morogoro pamoja na Rukwa ikiwa ni mchango wa Serikali ya Marekani katika kuisaidia Serikali ya Tanzania kufikia lengo la kupunguza tatizo la udumavu kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano kutoka asilimia 34 hadi asilimia 28 ifikapo mwaka 2021.

Akitoa salamu za mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo alitaja baadhi ya mambo yanayopelekea wananchi wa Mkoa wa Rukwa, hususan watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kuwa na hali duni ya lishe huku akisistiza Utamaduni na mazoea ya wananchi wengi kutumia aina fulani za vyakula hususan nafaka kwa muda mrefu bila kuchanganya na makundi mengine ya vyakula, hivyo kukosa virutubishi muhimu.

“Wananchi wengi hasa wanaoishi Vijijini kutokuwa na Elimu ya kutosha kuhusu masuala ya lishe bora.Baadhi ya akinamama na familia kwa ujumla, kutozingatia taratibu za unyonyeshaji na ulishaji bora kwa watoto wenye umri chini ya miaka miwili. Baadhi ya akina mama wenye watoto wadogo kukosa muda wa kutosha wa kuwahudumia watoto wao kwa lishe bora,” Alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirila la Maendeleo la Watu wa Marekani Andrew Karas aliishukuru serikali kwa kuweka kipaumbele juhudi za kuhakikisha inapunguza hali ya udumavu nchini kwa kutekeleza afua mbalimbali kuanzia ngazi ya kitaifa hadi kwenye halmashauri huku akimpongeza mgeni rasmi wa shughuli hiyo Mh Suleima Jafo na Wizara ya TAMISEMI kwa kutoa kipaumbele maboresho ya lishe.

“Sisi sote tunatambua mchango wa Lishe katika maendeleo jumuishia na maendeleo endelevu, tunavyojua Tanzania inaendelea kukumbwa na viwango vya juu vyua utapiamlo Mkoani Rukwa zaidi ya nusu ya watoto waliochini ya miaka mitano wana udumavu ambayo ni asilimia kubwa zaidi nchini, utapiamlo una athari mbaya kwa mtu binafsi, familia na taifa, unaathiri maendeleo ya Kimwili na pia kiakili, lishe duni huchangia kuwa na uwezo mdogo wa kujifunza,” Alisema.

Mradi huu unalenga kuongeza na kuboresha upatikanaji na utoaji wa huduma bora za lishe katika vituo vya afya na jamii, uzalishaji na ulaji wa vyakula vyenye virutubishi kwa wingi katika ngazi ya kaya, udhibiti wa usawa wa kijinsia katika mapato na matumizi ya rasilimali za nyumbani ili kuhakikisha upatikanaji wa vyakula mchanganyiko.

Shirika la maendeleo la Watu wa marekani limetenga zaidi ya dola za kimarekani milioni 19 ili kutekeleza mtadi wa lishe Endelevu kwa kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2018 hadi 2022 katika Mikoa minne na Halmashauri 22 za Tanzania Bara na kulenga kufikia zaidi ya wanawake milioni 1.5 walio katika umri wa kuzaa, watoto milioni 1.1 walio chini ya umri wa miaka mitano na vijana walio katika rika la baleghe 330,000 wenye umri wa miaka 15-19.