NEWS

2 Oktoba 2019

Puma yamuunga mkono RC Makonda, yatoa shilingi 40 milioni upasuaji moyo watoto 20


Kampuni ya mafuta ya Puma Energy, imeunga mkono kampeni ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ya kuokoa maisha maisha watoto wanaogua ugonjwa wa moyo kwa kuchangia shilingi milioni 40 ili kufanikisha upasuaji kwa watoto 20.

Hayo yamebanishwa Mkurugenzi wa Puma Energy, Dominic Dhanah, alizungumza jana wakati wa mashindano ya michoro ya usalama barabarani kwa wanafunzi wa mkoa wa Dare es Salaam kwa mwaka 2019.

“Hatua ya kuunga mkono kampeni hiyo ni kuhakikisha wanaokoa maisha ya watoto ambao wazazi wao hawana uwezo wa kugharamia matibabu,” amesema.

Kuhusu mafunzo ya usalama barabarani kwa watoto wa shule za msingi, amesema yamesaidia kupunguza ajali katika maeneo ambayo wametoa mafunzo hivyo wanaamini kwa kufanya hivyo wanaokoa kizazi cha sasa na kijacho kwa kuwa elimu ya matumizi bora ya barabara inaendelea kusambaa.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amesema kuwa Kampuni ya Puma, imetoa kiasi cha Shilingi milioni 40 kwa ajili ya kugharamia matibabu ya watoto 20 ambao wanahitaji kufanyiwa upasuaji wa moyo lakini wazazi mwao hawana uwezo wa kulipia matibabu.

“Puma wameonesha njia ya kujali na kutusaidia kwenye moyo. Niliomba msaada huo katika mkutano wa SADC. Nina watoto 500 pale Muhimbili wanaumwa moyo.

“Mimi nikialikwa mahali ninaomba msaada kwa wananchi wangu. Dominick wa Puma nilimuomba. Gharama za matibabu kwa kila mtoto ni shilingi milioni mbili. Kwa kiasi hiki cha fedha shilingi milioni 40 sasa tunakwenda kurudisha tabasabu kwa watoto 20.

“Hata nilipokutana na Balozi wa Dubai baada ya kumueleza hili, yeye alikwenda kuleta madaktari ambao walifanya upasuaji wa matibabu kwa watoto 50. Mwezi ujao nitaunda kamati ya watu saba kwa ajili ya kusaka shilingi bilioni moja, ili mpaka tukifika Desemba mwaka huu watoto wote wawe wamefanyiwa upasuaji,” alisema RC Makonda