NEWS

3 Oktoba 2019

WANANCHI WAZUA TIMBWILI SERIKALI YA MTAA

WAKAZI wa Mtaa wa Kisiwani, Magomeni – Mikumi, jijini Dar, wameibua timbwili la aina yake ofisini kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, kuzuia ujenzi wa ukuta ambao unaziba njia wanayoitumia. 

 

Waandishi wa Uwazi walifika katika eneo la tukio, lililotokea mwishoni mwa wiki iliyopita na kufanikiwa kuzungumza na wananchi hao (pichani ukurasa wa nyuma) ambao walisema wanashangazwa na uamuzi wa mtu waliyemtaja kwa jina la Haji Mbabe kutaka kujenga ukuta kwenye uchoro ambao wanautumia.

 

WAFUNGUKA NA UWAZI

Omari Mambo alikuwa wa kwanza kuzungumza na Uwazi, ambapo alisema: “Ndugu waandishi, huyu bwana Haji Mbabe anatushangaza sana. Unajua amenunua hiyo nyumba kama miezi mitano iliyopita, ghafla amezungusha mabati, anataka kuanza ujenzi wa ukuta.

 

“Miaka yote tunatumia hiyo njia kwa shughuli za kijamii, kama kupeleka wagonjwa hospitali, kupitisha maiti nk, sasa leo anataka kuziba. Sisi tutapitia wapi? Hakuna uungwana wa namna hii.

“Sasa kwa sababu tumesikia amesema alipewa kibali na serikali ya mtaa, ndiyo maana tumeamua kuja hapa kwa mwenyekiti ili tujue moja. Kila siku anatutisha, kwamba hapa atajenga na hatuna cha kumfanya.

 

“Tunachotaka haki itendeke, aache huu uchochoro uendelee kufanya kazi kama ilivyokuwa mwanzo kwa sababu kwa sasa tunapata sana shida, hata ikitokea nyumba imeungua huku gari ya zima moto haliwezi kupita, sasa tutaishije?”

 

Akizungumza kwa uchungu, Nuru Ahmad, huku akisema: “Kiufupi tumechanganyikiwa, hapa nilipo namuuguza mama yangu, yupo hoi kitandani na pale ndiyo sehemu ambayo huwa tunaitumia kumpitishia wakati wa kumpeleka hospitali. Sasa akiziba tutashindwa kumpeleka mama hospitali.”

 

POLISI WATINGA ENEO LA TUKIO

Uwazi lilifika hadi eneo ambalo ukuta huo unatakiwa kujengwa, ambapo simulizi nyingine ilieleza kuwa askari walifika eneo hilo na kuwatawanya wananchi, kama inavyosimuliwa na Kasimu Ally:

 

“Hivi tunavyokuambia Polisi wametoka hapa muda sio mrefu, tena wamesema wanarudi kwa mara nyingine. Wamekuja hapa na silaha mkononi ili tuache huyo tajiri ajenge huu ukuta lakini sisi kama wananchi tutahakikisha tunaungana kwa pamoja na huo ukuta hautajengwa.“

KAULI YA MWENYEKITI

Uwazi lilimuweka kati, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mikumi, Bakari Ramadhani Katubi ambaye alikiri kutokea kwa tukio hilo mtaani kwake na kueleza kwamba Mbabe alinunua nyumba eneo hilo miezi mitano iliyopita. Anasema, hivi karibuni alipokea barua kutoka kwa Mbabe, kupitia kwa Amosi ambaye ni kijana wake, kuomba kujenga ukuta katika uchochoro huo, ambapo alisaini kupokea kwa barua hiyo.

 

“Nilipokea barua ya huyu bwana (Haji) na nilisaini kuipokea, ila siyo kumruhusu kujenga. Nimeshangaa tayari ameshaleta mafundi, tayari kwa kujenga, jambo ambalo ni kosa kisheria,” alisema Katubi.

 

Akaongeza: “Kipindi ananiletea hiyo barua, nilimwambia kuwa haiwezekani na nikamtajia madhara yatakayotokea kwa kuwa ile ni njia ya watu, kupitisha wagonjwa na hata magari ya zimamoto, magari ya kunyonya uchafu nk. Lakini amekaidi.”

 

Jitihada za kumpata Mbabe kuzungumzia madai hayo ziligongwa mwamba, lakini bado juhudi za kumsaka zinaendelea. Tutawaletea kinachoendelea baada ya kupatikana.

The post WANANCHI WAZUA TIMBWILI SERIKALI YA MTAA appeared first on Global Publishers.