NEWS

5 Novemba 2019

Aibu ya mwaka Mke amfumania LIVE mumewe na denti gesti

TANGU mwaka huu wa 2019 umeanza kuna matukio mengi yametokea, lakini hili limebeba aibu nzito zaidi, Gazeti la Ijumaa Wikienda lina ishu nzito.

Aibu hiyo imempata mume wa mtu aliyetajwa kwa jina la Filbert Sunamie, mkazi wa Kibada, Kigamboni jijini Dar, twende taratibu!

Iko hivi, Sunamie amejikuta akifedheheka baada ya kufumaniwa laivu na mkewe akiwa na denti kwenye chumba cha nyumba ya kulala wageni (gesti).

ENEO LA TUKIO

Tukio hilo lilijiri kwenye nyumba hiyo ya kulala wageni iliyopo Sinza-Madukani jijini Dar, majira ya saa 9:00 usiku wa kuamkia Ijumaa iliyoita.

Sunamie aliyetajwa kuwa mfanyabiashara mkubwa hapa nchini alinaswa na mkewe aliyejitambulisha kwa jina moja la Shani ambaye aliambatana na polisi waliokuwa na difenda.

Awali, wakiwa katika ratiba zao za kukamilisha majukumu yao ya kihabari, wanahabari wetu walipata taarifa za kuwepo kwa tukio hilo dakika chache kabla ya kufanyika.

WANAHABARI WETU WATINGA

Walichokifanya wanahabari wetu ni kujiweka sawa kisha kutinga eneo la tukio ndani ya dakika sifuri na kuungana na msafara wa polisi na mke aliyekuwa amepagawa kutokana na uhakika aliokuwa nao kwamba mumuwe huyo alikuwa chumbani na denti huyo.

KABLA YA FUMANIZI

Kutokana na kuwa na hamu ya kutaka kujua kilichokuwa kinaenda kujiri, wanahabari wetu ilibidi waulize kama mama huyo alikuwa na uhakika wa kuwepo kwa fumanizi hilo.

“Huyo binti ambaye mume wangu yupo naye chumbani ni mjukuu wangu. Ni mjukuu wa dada yangu kabisa hivyo na sisi ni mjukuu au mtoto wetu na ana umri wa miaka 19.

“Huyo binti yupo kidato cha nne na anaanza mitihani ya form four Jumatatu (leo).

“Kuhusu kujua kama mume wangu anatembea na mjukuu wetu, nimewafuatilia kwa muda mrefu na huyo binti alikuwa akiniambia kila kitu namna babu yake anavyomsumbua akimtaka kimapenzi.

“Huyu binti au tuseme mjukuu wangu anakaa Mwenge (Dar) maana ndiko anakosoma, lakini kule nyumbani (Kigamboni) huwa anakuja na kuondoka.

“Sasa leo nimeambiwa na watu wanaowajua kuwa mume wangu amemfuata huyo binti na anazurura naye kuanzia kule Msasani, tumepita huko kote hadi huku Sinza yupo na mjukuu wetu na sasa yupo naye chumbani gesti,” alisema mama huyo akiwa amepaniki ile mbaya.

TURUDI KWENYE FUMANIZI

Baada ya wanahabari wetu kuhakikishiwa na mama huyo kwamba tukio lipo, walihoji uhalali na kama taarifa hizo zimeripotiwa polisi ili kupata ulinzi kwani kwenye fumanizi lolote linaweza kutokea.

Wanahabari wetu walimshuhudia mama huyo akiingia kwenye gesti hiyo kisha kulitokea ubishani baada ya uongozi kutia ngumu kwa watu kuingia bila kibali.

Hata hivyo, ilibidi polisi wafanye kazi yao huku wakiwasiliana na wakubwa wao ambapo uongozi wa gesti hiyo ulitii. Baada ya hapo mama huyo alielekea kwenye chumba alichoelekezwa na watonyaji wake huku presha ikiwa juu.

Alipofika mlangoni aligonga kiujanja akijifanya mhudumu.

LA HAULA…

La haula! Ile mumewe anafungua tu mlango, akakutana uso kwa uso na mkewe aliyembatana na polisi waliomsindikiza kufanya fumanizi hilo matata.

Mume huyo, baada ya kugongana uso kwa uso na mkewe, fasta alirudi ndani na kuanza kuvaa nguo harakaharaka huku binti yeye akiwa hajavua nguo hata moja.

MADIKODIKO KAMA YOTE MEZANI

Mke huyo alijikuta akipigwa butwaa baada ya kupiga jicho chumbani humo na kutoamini macho yake. Alipopiga jicho juu ya meza alikutana na mabaki ya madikodiko kama yote waliyokuwa wamekula yakiwemo ya samaki mkubwa aina ya sato kutoka jijini wa Mwanza na juisi baridi za matunda.

KILIO UTADHANI MSIBA

Katika kile kilichoonekana kumuumiza bibi huyo, alijikuta akiangua kilio utadhani kuna msiba na kuanza kuelezea mambo yao ya ndani. “Jamani ninyi wanaume ni watu wabaya sana. Jamani huyu ni mume wangu kabisa na huyu ni mjukuu wa dada yangu ambaye na mimi ni bibi yake kabisa. Pia huyu mume wangu naye ni babu yake.

“Sasa huyu baba jamani iweje amlete mjukuu wangu huku kwenye nyumba ya wageni na kukodi chumba cha gharama kubwa kama hii wakati siku mbili hizi alikuwa ananiambia mambo yake hayajakaa sawa?

“Mbaya zaidi huyu mjukuu wetu anatarajia kufanya mtihani wa kidato cha nne hapo keshokutwa tu (kuanzia leo) sasa kwa hali kama hii si anataka kumharibu mjukuu huyu baba jamani?

FULL KUTOA RISALA

“Ninyi wanaume kuweni na huruma basi jamani, ewe mume wangu nimekukosea nini mimi mkeo mpaka unidhalilishe kiasi hiki? Roho inaniuma sana jamani sijui nifanye nini?

“Huyu mume wangu kila kitu ninamfanyia, ninamfulia nguo, ninampikia, nimetoka naye mbali, lakini sijui ni shetani gani anamzuzua!” Alilia mama huyo kwa kuomboleza.

MUME ATAKA KULETA TAFRANI

Hata hivyo, mume huyo alitaka kuleta tafrani lakini hata hivyo alitulizwa na polisi waliokuwa wamejiweka sawa hivyo akawa mpole.

Wakati mama huyo akiomboleza kwa kilio polisi walimchukua yeye, mumewe na mjukuu huyo na kwenda nao Kituo cha Polisi cha Oysterbay jijini Dar kwa ajili ya maelezo zaidi.

KAMANDA WA POLISI

Kufuatia tukio hilo, Gazeti la Ijumaa Wikienda lilizungumza na Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi (ACP) Mussa Taibu na kumuuliza kinachoendelea kwenye sakata hilo ambapo kamanda huyo alisema halijamfikia mezani kwake.

Hata hivyo aliahidi kulifuatilia na kurudisha majibu. Alipopigiwa simu baadaye na kuulizwa kama alishalifutilia sakata hilo alimuomba mwanahabari wetu amuache na kusema alikuwa sehemu hatari. “Dah! Unajua niko sehemu ya hatari hebu naomba niache,” alisema Kamanda Taibu.

KUTOKA KWA MHARIRI

Gazeti la Ijumaa Wikienda linaahidi kulifuatilia sakata hilo hadi mwisho hivyo ni jukumu lako msomaji kufuatilia gazeti hili na mengine Pendwa ya Global Publishers -Mhariri.  Ili kutazama video za tukio hili, tembelea GlobalTV kwenye YouTube.

 

STORI: RICHARD BUKOS NA NEEMA ADRIAN, DAR

The post Aibu ya mwaka Mke amfumania LIVE mumewe na denti gesti appeared first on Global Publishers.