NEWS

3 Novemba 2019

Jinsi ya kujinasua na kizingiti cha ndugu, wazazi kwenye mahusiano!

MOJA kati ya changamoto ambayo vijana wa siku hizi wanakutana nayo ni kitendo cha wazazi kukwamisha mipango ya vijana wao. Upande wa mke unaweza kuwa umeridhia, lakini upande wa mume ukawa haujaridhia.  Hapo ndipo wapendanao wanapokutana na mtihani mzito. Hawajui nini cha kufanya, wanashindwa kung’amua wachague bega gani. Wawasikilize ndugu au wasikilize mioyo yao.

Hakika kila mmoja wetu anatambua umuhimu wa wazazi. Wazazi ndio wametuleta duniani, ukisoma vitabu vya dini vinatuelekeza kwamba wao ndiyo wana nafasi ya pili ya ‘ki-mungu’ hapa duniani. Wazazi ndio wametangulia kuliona jua. Wao wana uzoefu mkubwa wa maisha. Kwanza maisha yao wenyewe lakini pili, wamejifunza kupitia maisha ya watu wengine.

Hivyo kwa namna moja ama nyingine, wanaweza kuona tatizo kabla halijatokea na wakakushauri kitu cha kufanya hata katika masuala yako ya uhusiano. Wazazi wanaweza kukufundisha busara za maisha, wanaweza kukueleza nini cha kufanya pindi unapokutana na changamoto fulani katika mahusiano yako.

Haifai kuwapuuza hata kidogo wazazi. Unatakiwa kuwasikiliza tena kwa wakati ili uweze kuishi katika misingi yenye maadili na kutojikuta matatizoni. Tatizo la vijana wengi wa sasa huwa hawafanyi maisha na wake au waume wema, wanapenda kufanya maonesho ya wake au waume zao.

Mwanamke anataka kuolewa na mtu, kwa sababu tu ana fedha au ni ‘handsome’. Mwanaume naye vivyo hivyo, anataka tu kuoa kwa sababu aliye naye ni mrembo sana. Wazazi wetu hawakuyaangalia sana hayo. Kikubwa walikuwa wakitazama mapenzi ya kweli, walitazama zaidi utu na si kitu. Hapo ndio maana nasema wazazi wetu waliona mbali katika suala zima la maisha ya mahusiano.

Hivyo basi, kabla ya kuingia kwenye uhusiano na mtu, hakikisha huyo unayeanzisha naye uhusiano ana upendo wa kweli kwako. Hakikisha ana utu, tabia nyingine ndogondogo mnaweza kubadilishana mkiwa ndani, lakini kubwa la kulitazama ni mapenzi ya dhati na utu.

Mtu kama hana mapenzi ya dhati ni bora ukaachana naye mapema. Kama hana utu, haifai kuishi naye maana mtapoteza muda bure na baadaye mtaishia pabaya. Ikitokea tayari mmeingia kwenye uhusiano mzito na mkajihakikishia kwamba kweli mnapendana na utu upo kati yenu, halafu kukawa na kikwazo cha wazazi au ndugu, hampaswi kupaniki.

Mnatakiwa kuyaheshimu mawazo yao lakini muyachuje kulingana na uzito wa uhusiano wenu. Kila mmoja amtafakari mwenzake, ana mapenzi ya dhati ana utu? Mkishapata jibu, liwekeni kwenye mizani na yale ya wazazi au ndugu. Mkibaini kwamba utu na mapenzi yenu ni makubwa kuliko ushauri wao, chukueni muda mzuri wa kujinasua katika kizingiti hicho.

Upande unaoleta kizingiti, mhusika kati yenu abebe jukumu la kuwaelewesha juu ya upendo na utu mlionao. Kwa kutumia lugha ya kistaarabu, awaeleweshe kwamba wewe ndiye chaguo lake na anauona upendo wa dhati kwako. Kama hakuna madhara yoyote, wakupe kibali cha kuoana na mtu umpendaye kwani kwa kufanya hivyo watakufanya uishi vizuri kwa raha mustarehe kuliko kuoa au kuolewa na mtu ambaye hamjaendana kiutu, au hamjapendana.

Hakika wataelewa hata kama si kwa haraka, lakini kadiri siku zinavyozidi kwenda, watakuelewa na watakupa baraka zao. Tukutane wiki ijayo. Unaweza kunifuata kwenye mitandao yangu ya kijamii, Instagram na Facebook natumia Erick Evarist, Twitter natumia ENangale.

The post Jinsi ya kujinasua na kizingiti cha ndugu, wazazi kwenye mahusiano! appeared first on Global Publishers.