DAR: Usiombe kuhadhitiwa utakapopata bahati ya kuhudhuria ndoa ya mwanamuziki wa Bongo Fleva, Vanessa Hau Mdee ‘Vee Money’ (31), ambaye sasa amemnasa staa bilionea Mmarekani, Olurotimi Akinosho ‘Rotimi’ (30), IJUMAA linakupa zaidi.
PENZI LIMECHIPUA
Tayari wawili hao wamethibitisha kuwa kwenye penzi zito ambalo limechipua mithili ya maua wakati wa masika na kumlazimu Vanessa kuweka wazi kuwa sasa penzi hilo limemfanya anenepe. “Nilipomuona tu mpenzi wangu wa sasa Rotimi, nikajua nimepata mume wa kuishi naye maisha yangu yote,” amesema Vanessa.
Licha ya kwamba sasa safari za Vanessa au Cash Madam kutoka Bongo kuelekea Miami, Marekani hazikauki.
“Kwa mwezi ninakuwa Bongo kama siku kumi hivi, nyingine nakuwa nje,” amesema Vanessa. Mrembo huyo ameeleza kuwa katika uhusiano alionao sasa ndiyo unatarajiwa kutamanisha ndoto za wanawake wengi kwani kifuatacho ni kishindo kikubwa cha ndoa.
Katika ndoa hiyo, imeelezwa kuwa na kishindo cha kipekee kutokana na staa huyo wa Marekani kuwa na mkwanja wa kutosha.
UTAJIRI KAMA WA MONDI
Kwa mujibu wa mitandao ya Wikipedia, Forbes, IMDb na mitandao mingine mbalimbali, Rotimi anakadiriwa kuwa na utajiri wa Dola za Kimarekani milioni tano (zaidi ya shilingi bilioni 11.5) unaolingana na wa staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Mondi’.
Hata hivyo, utajiri wake umeelezwa kukua kwa kasi kutokana na kazi mbalimbali za kisanaa anazozifanya ikiwamo, uigizaji, Tamthiliya ya Power na shoo mbalimbali ikiwamo uimbaji wa miondoko ya RnB na kwamba mwaka 2018 alikuwa na utajiri wa Dola za Kimarekani 100,000, lakini sasa umekua kuanzia Januari na kukadiriwa kufikia milioni tano mwaka huu.
KISHINDO NDOA YA VANESSA
Kishindo cha ndoa ya Vee Money kinatarajiwa kuchagizwa na mastaa maarufu wa Marekani, akiwemo rapa nguli, 50 Cent ambaye ni bosi wa Rotimi kwa kuwa amemsainisha katika lebo yake ya G-Unit, lakini pia rapa huyo ndiye mkurugenzi wa uzalishaji wa tamthiliya maarufu ya Boss.
MASTAA WAKUBWA
Mbali na 50 Cent, mastaa kibao wa Marekani kama vile Jayz, TI na Keyshia Cole ambaye amemshirikisha Rotimi katika moja ya video yake ni baadhi ya mastaa ambao huwezi kuwaweka kando katika shughuli hiyo.
ROTIMI NI NANI?
Rotimi ambaye ni mhitimu wa Shahada ya Mawasiliano na Biashara, kwa uchache amezaliwa Novemba 30, 1988 nchini Marekani na wazazi wake ambao wote wana asili ya Nigeria.
Kwa sasa ana uraia pacha wa Marekani na Nigeria, lakini pia umaarufu wake umekua maradufu kutokana na Tamthiliya ya Boss ambayo inabamba akitumia jina la Darius Morrison wakati katika tamthiliya nyingine ya Power anaitwa Andrew Coleman.
MAISHA NA ELIMU
Rotimi alizaliwa Maplewood, New Jersey nchini Marekani, kwa wazazi wenye asili ya Nigeria; baba yake ni mwekezaji katika Benki ya Yoruba (Nigeria) na mama yake ambaye anatoka katika Kabila la Igbo- Nigeria, alikuwa pia mfanyakazi serikalini.
Rotimi alimaliza elimu ya juu katika Shule ya Columbia ambapo ambapo pia alikuwa mchezaji mahiri wa mpira wa kikapu na mwimba kwaya.
Hata hivyo, aliendelea na masomo yake katika Chuo Kikuu cha Northwestern na kuhitimu na Shahada ya Mawasiliano na Biashara mwaka 2010.
UIGIZAJI
Katika tasnia ya uigizaji, kwa mara ya kwanza alijaribiwa katika Tamthilia ya Boss ambapo aliigiza kama muuzaji dawa za kulevya. Lakini pia alipata kuonekana kwenye episodi tatu za Tamthiliya ya Betrayal kwenye Televisheni ya ABC.
Rotimi aliendelea kutengeneza jina katika Filamu ya Black Nativity (2013) na kufuatiwa na Imperial Dream –ambayo baada ilikuja kushinda Tuzo ya Best of NEXT katika tamasha la filamu lijulikanalo kama Sundance Film Festival.
Baadaye alionekana katika filamu kali ya Divergent (2014). Mwaka 2016, Rotimi pia aliigiza katika Sinema ya Deuces pamoja na Lance Gross na Larenz Tate.
Aliongezwa kwenye kikundi cha mastaa wa Tamthilia ya Power anakojiita jina la Andre Coleman.
MUZIKI
Rotimi ni msanii wa miondoko ya R&B. Machi 8, mwaka 2011 alitoa wimbo wenye jina la The Resume na mwaka huohuo, Novemba 30, akaachia While Tou Wait. Video za nyimbo hizo zilishirikisha wasanii mbalimbali wa Marekani na kampuni kubwa za habari za kiburudani kama vile MTV, MTV Base na VH1 Soul.
JUKWAA MOJA NA T.I
Rotimi amepafomu katika jukwaa moja na Jennifer Hudson, T.I, Estelle na NERD; pia alipafomu katika shoo kubwa za BET na Park. Aidha, alionekana kwenye video ya mwimbaji maarufu wa R&B, Keyshia Cole ijulikanayo kama Trust and Believe ambako aliigiza kama mchumba Cole.
Mwaka 2015, Rotimi, mbali na kuwa staa katika Tamthilia ya Boss ambayo msanii nguli na rapa maarufu, 50 Cent ndiye mkurugenzi mzalishaji, pia rapa huyo alimsainisha Rotimi katika lebo yake ya G-Unit. Rotimi aliachia wimbo wake wa kwanza chini ya 50 Cent uitwao Lotto.
2016 aliachia ngoma nyingine ya Doin It, katika moja ya ngoma zake tano ambazo mwaka 2017 aliachia albam iliyopewa jina la Jeep Music Vol.1.
Mwaka huu, ameachia singo moja yenye jina la Love Riddim ambayo imevutia mashabiki wengi wa muziki wa zamani na wa sasa.
MITINDO
Rotimi ndiye balozi na msemaji wa mradi wa shoo za fasheni zinazoandaliwa na rapa T.I. kama vile AKOO Clothing 2012 Spring/Summer Campaign, Aprili 2, 2012.
MRITHI WA BOB MARLEY
Katika mahojiano na stesheni moja ya huko nchini Marekani, Rotimi alizungumza kuhusu uasili wake kutoka Nigeria na Marekani na magumu mbalimbali aliyopitia mama yake.
Alisema; “Wazazi wangu walikuja Marekani walipokuwa na umri kama miaka 28. Mama yangu alikuja, hakuwa na makazi. Alihitimu masomo yake ya udaktari na nimekuwa sehemu ya ndoto yake kutokana na kujituma kwangu kwa bidii.”
Aliendelea kufafanua kuwa, mama yake alimwambia alitambua kuwa mwanaye atajiingiza kwenye biashara za masuala ya burudani kabla ya kuzaliwa.
“Mama yangu ni askari mashuhuri na shujaa. Kwa sababu alikuwa na nguvu za kiroho, aliniambia wakati akiwa mjamzito aliota ndoto akiwa na Bob Marley ambaye alimwambia ‘mtoto wako atakuwa mrithi wangu.”
UHUSIANO
Awali, ilifahamika kuwa Rotimi ana uhusiano wa kimapenzi na modo wa Instagram, Christina Rogers. Hata hivyo, licha ya kwamba uhusiano huo hakuwahi kuwekwa wazi kabla ya hivi karibuni jamaa huyo kutangaza kuwa na uhusiano wa kimapenzi Vanessa.