KUNA asilimia kubwa kwa mwanamke kuweza kujua siku zake za hatari za kupata ujauzito japo pia, wapo wengine ambao huwa hawajui vizuri mpangilio wa siku zao na kujikuta wamepata ujauzito katika wakati ambao wao wenyewe hawajapanga kufanya hivyo. Hapa ndipo tunapopata tatizo la mimba zisizotarajiwa. Si baba, wala mama ambaye anakuwa amefikiria kupata mtoto, lakini inatokea na wanajikuta hawana namna, wanalazimika tu kulea mimba na baadaye mtoto.
Hapa yawezekana kabisa ikawa mwanaume hayupo tayari kuzaa na huyo mwanamke, alikutana naye tu kimagumashi na hana mpango naye, lakini wamejikuta tu wamepata mtoto. Vivyo hivyo kwa mwanamke, amenasa ghafla tu kwa mwanaume ambaye pengine hakuwa na malengo naye.
Nini kitatokea hapa? Kwa kuwa nyote wawili hamkuwa na malengo ya kuwa pamoja, basi kinachofuata hapo ni changamoto nyingi za kulea mtoto ambaye hamkuwa mmejiandaa kuwa naye. Mbali na kujiandaa kumlea, ninyi wenyewe hamkuwa na mtoto amlee, lakini tatizo linahamia kwa mwanamke wake mpya.
Unakuta naye hawezi kuwa na mapenzi ya dhati kwa yule mtoto wako. Huu ndiyo ukweli japokuwa wapo baadhi ya wanawake wanaoweza kuwalea watoto wa aina hiyo bila shida yoyote, lakini wengi wao hawawezi. Watawanyanyasa tu, nyumba haiwezi kuwa na amani.
Marafiki, tunapaswa kulifahamu jambo hili na kulichukulia hatua kabla mambo hayajaharibika. Unapoingia kwenye uhusiano na mtu, hakikisha upo ‘serious’ na huo uhusiano. Usibahatishe bahatishe halafu ukaanza kushiriki tendo la ndoa na mtu ambaye bado humuelewielewi.
Ni hatari kuishi kwa kujaribujaribu kwa sababu wakati upo kwenye hayo majaribio, lolote linaweza kutokea halafu mkajikuta kwenye matatizo ambayo nimeyaainisha hapo juu. Mtu humpendi na humuhitaji katika maisha yako ya nini kushiriki naye tendo la ndoa?
Kama kwenye akili yako umeshajua kwamba huyu hamuendani, kwa nini mshiriki tendo? Hauoni kama unapoteza muda wako? Hauoni kama unakaribisha tatizo kubwa huko mbeleni kutokana na suala zima la malezi?
Sikia, ni vizuri ukazaa na mtu ambaye kweli unampenda. Achana na kuamini katika bahati mbaya, mtu kama huna malengo naye achana naye. Usiruhusu ukaribu ambao hauna mwisho mzuri halafu baadaye mje kuachana mkiwa tayari na mtoto.
Malezi mazuri ya watoto siku zote ni yale ya wazazi wote kulea kwa pamoja. Mnapochanganya malezi, ndipo linapokuja kuwa tatizo kubwa kwa mtoto wenu. Liepuke hilo kabla halijatokea, chaguo lako la kwanza liwe ni kuishi na mtu ambaye kweli unampenda na ndiye wa maisha yako.
Ni hayo tu kwa leo, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine murua. Waweza kunifuata kwenye mitandao yangu ya kijamii; Instagram na Facebook: Erick Evarist, Twitter: ENangale.
The post KUZAA BILA MPANGO NI TATIZO JIFUNZE appeared first on Global Publishers.