KOCHA Mkuu wa Simba, Mbelgiji, Patrick Aussems ameshtushwa na kitendo cha uongozi wa Yanga kuvunja mkataba na aliyekuwa kocha wake, Mwinyi Zahera lakini akasisitiza hawezi kujali kwa kuwa wapo kwa ajili ya kufukuzwa.
Aussems ametoa kauli hiyo ikiwa ni muda mchache tangu uongozi wa Yanga kutangaza kuachana na kocha huyo raia wa DR Congo ambapo nafasi yake imezibwa kwa muda na Charles Boniface Mkwasa.
Yanga imevunja benchi lote la ufundi lililokuwa likiongozwa na Zahera baada ya kufanya vibaya katika Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kutolewa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika na Pyramids ya Misri kwa jumla ya mabao 5-1.
Akizungumza na Championi Jumatano, Aussems alisema kuwa ameshtushwa na taarifa hizo lakini haziwezi kutibua mipango yake kwa kuwa ni kitu asichoweza kuhusika nacho na makocha kutimuliwa ni kawaida sana.
“Binafsi sina hizo taarifa ndiyo kwanza nasikia kwako, nimeshtuka ingawa siwezi kuharibu chochote kwa sababu zaidi napaswa kuangalia timu yangu inafanya kitu gani kutokana na malengo yetu.
“Unajua suala hilo kwa makocha ni jambo la kawaida kutokea, usishangae kupendwa pale timu inapokuwa inafanya vizuri lakini inapokuwa imeharibu mambo yote yanakwenda tofauti, hivyo tupo hapa ili tutimuliwe,” alisema Aussems.
Ibrahim Mussa na Iddy Nonga
The post Mbelgiji Simba: Acha Zahera Aende Zake appeared first on Global Publishers.