NEWS

24 Novemba 2019

Mfahamu Muwekezaji Aliyeishika Bombardier Nchini Canada


Hermanus Phillipus Steyn Ni muwekezaji anayejikita zaidi katika kilimo. Aliwekeza nchini kwa kutumia kam-puni yake ya Rift Valley Seed Company Limited.

Lakini mali zake zikataifishwa na Serikali mwaka 1982 na anadai kuwa wakati huo walifikia makubal-iano ya fidia. Alianza kulipwa na Serikali ya Awamu ya Nne na malipo yaliposimama aliamua kuomba kukazia makubaliano yaliyotokana na amri ya mahakama ya Tanzania.

Hata hivyo, Serikali ilimshinda baada ya kujenga hoja kuwa mahakama hiyo ilikosea katika kufikia uamuzi kwa kuwa haina mamlaka hayo. Steyn pia alihusika katika sakata la kugombea ardhi nchini Kenya dhidi ya watu wapatao 200 wa kabila la Wamasai.


Hermanus Steyn aliyefungua kesi nchini Afrika Kusini na kusababisha ndege ya Tanzania aina ya Airbus A200-300 kuzuiwa, amezuia tena ndege mpya aina ya Bombardier Q400 nchini Canada, na tayari Serikali imejiandaa kupambana naye tena.

Hii ni mara ya tatu kwa ndege ya Tanzania kuzuiwa kutokana na amri ya mahakama baada ya ndege ya kwanza kuzuiwa nchini Canada wakati ikijiandaa kuja nchini baada ya kununuliwa na Serikali, na nyingine aina ya Airbus 220-300 kuzuiwa Afrika Kusini ambako Steyn aliomba kukaziwa kwa maamuzi ya shauri lililoamuliwa na Mahakama ya Tanzania.

Hata hivyo, Serikali ilifanikiwa kukomboa ndege hizo, ikiwa imejenga hoja Afrika Kusini kuwa amri ya kuzuia ndege ilitolewa kimakosa na mahakama hiyo kwa kuwa haina mamlaka ya kukazia hukumu iliyotolewa na mahakama nyingine ya nje ya Afrika Kusini.

Na kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Palamagamba Kabudi, Steyn alikata rufaa nchini Afrika Kusini na wiki iliyopita alishindwa na hivyo kuamua kukimbilia Canada.

“Jambo linalosikitisha ndege kutoka Marekani, Dreamliner mbili, hazikushikwa, zimefika. Lakini kila ndege inapotakiwa kuondoka Canada, tunashangaa hao watu, matapeli wanajuaje na ndege zinakwenda kukamatwa?” alisema Profesa Kabudi katika hafla ya kuapisha mabalozi iliyofanyika Ikulu jijini Dodoma.

Steyn, mwekezaji ambaye mali zake zilizokuwa chini ya Rift Valley Seed Company zilitaifishwa mwaka 1982, anataka Serikali imlipe fidia ya takriban dola 33 milioni, ikiwa ni pamoja na riba, kama ilivyokubaliwa wakati wa utaifishwaji huo na tayari alianza kulipwa na Serikali ya Awamu ya Nne.

Alifanikiwa kuizuia Airbus 220-300 iliyokuwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo jijini Johannesburg katika shauri alilofungua Mahakama Kuu ya Gauteng.

Hata hivyo, Serikali ilifungua shauri katika mahakama hiyo dhidi ya wajibu maombi wanane, akiwemo Steyn, Kampuni ya Viwanja vya Ndege vya Afrika Kusini na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Afrika Kusini. Jaji katika shauri hilo akaamua kuwa mahakama hiyo haikuwa na mamlaka ya kutoa amri ya kuzuia mali kwa lengo la kuthibitisha uamuzi uliotolewa na mahakama ya nje na kuagiza Steyn alipe gharama za kesi, zikiwemo za kutumia mawakili wawili.

Jana Profesa Kabudi alimwambia Rais John Magufuli kuwa ndege nyingine iliyokuwa ije nchini, imekamatwa.

“Na aliyefanya hivyo, Mheshimiwa Rais, ni mtu yuleyule ambaye alikamata ndege yetu Afrika Kusini, tukaenda mahakamani tukamshinda,” alisema Profesa Kabudi.

“Amekata rufaa, Mheshimiwa Rais, na wiki iliyopita ameshindwa tena rufaa Afrika Kusini. Huyohuyo sasa amekimbilia Canada amekamata ndege ya Bombardier Q400.”

Profesa Kabudi alisema kuendelea kwa vitendo hivyo ni hujuma za mabeberu wasiofurahishwa na maendeleo ya Tanzania.

Kukamatwa kwa ndege hiyo nchini Canada kunaonekana kutikisa uhusiano baina ya nchi hiyo na Tanzania.

“Jana nilichukua hatua ya kumuita balozi wa Canada hapa nchini na alifika Dodoma ndio maana Mheshimiwa Rais mchana hukuniona kwenye shughuli hizo kwa sababu nilikuwa na mazungumzo naye marefu. Nimemwambia kinagaubaga, bila ya kupepesa macho, bila tashwishi kwamba hatufurahishwi kabisa kwa tabia na vitendo hivi vya kila ndege yetu inapotakiwa kuondoka Canada kurudi Tanzania inakamatwa,” alisema Profesa Kabudi.

“Na nimemwambia si tu kwamba tumesikitika, lakini tumekasirika na kwa maana hiyo tunafikiri--Mheshimiwa Rais utushauri-- kama Canada inaendelea kuruhusu vitu kama hivyo, siyo wao peke yao wanaotengeneza ndege.

“Hatukufanya makosa kwenda kununua ndege Canada. Ziko nchi nyingine. Hata Brazil wanatengeneza ndege.”

Profesa Kabudi alisema mbali na kumwita balozi huyo, hatua za haraka zimechukuliwa ili kuhakikisha jambo hilo linasimamiwa kwa kutafuta wanasheria nchini Canada ili kupigania ndege hiyo.

“Ninavyozungumza hivi pia wanasheria wetu pamoja na katibu mkuu wa uchukuzi wanatarajia kuondoka nchini kwenda huko kuungana na wanasheria wale ili kuhakikisha tunatetea ndege ili irudi,” alisema Profesa Kabudi.

Ndege ya kwanza, pia aina ya Bombardier ilizuiwa nchini Canada baada ya kampuni ya ujenzi ya Stirling Civil Engineering Ltd kufungua shauri la madai ya fidia ya dola 38 milioni za Kimarekani baada ya mkataba wake wa ujenzi wa barabara kukatishwa.

Mahakama ilitoa amri ya kuzuia ndege hiyo ambayo ndio kwanza ilikuwa inatoka katika kiwanda cha kampuni ya Bombardier Inc na tayari kuruhusiwa kuja nchini kutokana na shauri hilo.

Serikali iliamua kupambana mahakamani na baadaye ndege hiyo pamoja na nyingine mbili zikaja nchini na kukabidhiwa kwa Shirika la Ndege la Air Tanzania (ATCL).

Mbali na kutuma wanasheria, Serikali pia ilimuandikia barua Waziri Mkuu wa Canada ili asaidie kuharakisha shauri hilo.

Madai ya Stirling yalitokana na uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi ya mwaka 2010 kuhusu mkataba wa ujenzi wa barabara uliokatishwa.

Profesa Kabudi alihusisha kukamatwa huko kwa ndege za Tanzania na ubeberu.

Alisema mara nyingi Rais Magufuli alipokuwa anazungumzia suala la hujuma alikuwa hana uhakika, lakini sasa anaelewa kinachosemwa kwa kuwa kila juhudi zinapoongezwa katika kuleta maendeleo, wapo ambao wanakesha kukwamisha.

“Hao ni mabeberu nje lakini kwa kutumia na baadhi ya watu ndani ya nchi kwa faida zao za muda mfupi,” alisema Profesa Kabudi.

“Haiwezekani kila ndege inapokwenda kufanyiwa majaribio inasingiziwa hali ya hewa mbaya halafu baadaye inakamatwa.

“Unafanya juhudi kubwa ila wapo wanaokesha kukwamisha lakini maendeleo ya nchi hii ni kama simba aungurumaye.”

Mabalozi walioapishwa katika hafla ya jana ni Meja Jenerali Anselm Shigongo Bahati, ambaye anakwenda nchini Misri, Mohamed Abdallah Mtonga (Abu Dhabi), Jestas Abouk Nyamanga (Ubelgiji), Ali Jabir Mwadini (Saudi Arabia) na Dk Jilly Elibariki (Burundi).

Ubadhirifu Addis Ababa

Profesa Kabudi aliwataka mabalozi hao kusimamia vizuri fedha na mali katika nchi walizopangiwa.

Alisema udhaifu mkubwa katika balozi hutokana na usimamizi wa fedha na mali huku akitoa mfano wa ubalozi wa Ethiopia.