NEWS

4 Novemba 2019

 Tatizo la mtoto wa jicho! (cataract)-2

WIKI iliyopita tuliona namna ambavyo tatizo la mtoto wa jicho au cataract hutokana na kufanyika kwa ukungu katika lensi ya jicho. SASA ENDELEA…

DALILI

Dalili za mtu mwenye mtoto wa jicho au ukungu kwenye jicho huwa ni kati ya hizi zifuatazo; kuona ukungu au vitu vimefifia, kupata shida kuona wakati wa usiku, kuumizwa macho kwa mwanga, kuona nusu duara au duara kwenye mwanga unaong’aa au miale ya mwanga kama vile upinde wa mvua.

Kubadilisha mara kwa mara kwa lensi ya miwani kutokana na hali ya macho kuwa mbaya.

Kuona rangi zimefifia au rangi ya vitu kuwa ya njano, kuona kitu kimoja kwamba ni viwili katika jicho moja.

Mwanzo wa tatizo hili la ukungu kwenye lensi ya jicho huweza kudhuru sehemu ndogo ya jicho, kiasi kwamba hutapata dalili zozote, muda unapoendelea na ukungu huu kutanda kwenye sehemu kubwa ya lensi ya jicho, ndipo utakapoanza kupata dalili hizo.

Wakati gani uonane na daktari? Fanya mipango ya kuonana na daktari endapo unaona kuna mabadiliko yoyote katika macho yako kama kuona kitu kimoja kuwa mara mbili, kuona ukungu n.k.

Kupima; kujua kama una mtoto wa jicho, daktari atafanya vipimo vifuatavyo;

Kukuomba usome chati yenye maandishi makubwa na madogo ili kuona kiwango chako cha kuona, kitaalam huitwa visual acuity test. Jicho moja hufunikwa na baada ya kupimwa, hivyohivyo lingine hufunikwa na kupimwa kwa kutumia kifaa cha kamera na mwanga kuangalia jicho na lenzi ya jicho. Kifaa hiki kinajulikana kama microscopy, kutanua dirisha la jicho kwa ajili ya kuchunguza retina.

TIBA

Dawa aina ya matone inaweza kutolewa na daktari kwenye macho, inayosaidia kutanua mlango wa jicho na kumrahisishia kuona vyema kwa lensi ya jicho na baadaye atatumia kifaa kinachoitwa ophthaloscope na kuona kama kuna ukungu wowote au tatizo lingine.

Matibabu ya ukungu kwenye lensi ya jicho kwa njia ya upasuaji hutegemea maamuzi ya mgonjwa na daktari kwamba ni lini afanyiwe matibabu hayo.

Ukungu kwenye lensi ya jicho mara nyingi hausababishi matatizo yoyote na hata kama mtu akichelewa kufanyiwa matibabu, hakutadhuru uwezo wa kuona atakapofanyiwa upasuaji.

Matibabu ya tatizo hili hutegemea dalili alizonazo mgonjwa jinsi zinavyoathiri mfumo wa maisha yake kama kusoma au kuendesha gari wakati wa usiku. Mara baada ya kufanyiwa upasuaji, daktari atakuomba uwe unarudi kliniki ili kutathmini maendeleo yako.

Upasuaji wa kuondoa ukungu kwenye macho au cataract, hufanywa kwa kuondoa lensi iliyoharibika na kuweka nyingine bandia.

Lensi hii huwekwa mahali lensi ya asili ilipokuwa na mara baada ya kuwekwa, hukaa kwa muda wote unaoishi.

Kwa baadhi ya watu, baada ya kuondolewa kwa lensi asilia ya jicho, uwekaji wa lensi ya bandia hauwezi kufanyika, hivyo mtu atapewa miwani tu ili kumsaidia kuona.

Upasuaji wa kuondoa lensi hii ya asili na kuweka ya bandia, hufanyika kwa muda mfupi na mgonjwa anaweza kuruhusiwa siku hiyohiyo kwenda nyumbani.

Upasuaji unapokuwa unafanyika, mgonjwa anapewa ganzi sehemu ya jicho ili kutosikia maumivu, hivyo mgonjwa huwa macho wakati wote wa upasuaji.

Baada ya upasuaji, utajisikia hali isiyo ya kawaida, lakini baada ya siku chache na baada ya wiki nane utakuwa umepona kabisa. Kama una ukungu katika macho yote, basi daktari atapanga matibabu ya jicho lingine baada ya mwezi mmoja au miwili.

-MWISHO-

The post  Tatizo la mtoto wa jicho! (cataract)-2 appeared first on Global Publishers.