WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa 2020/2021 umelenga kutekeleza maeneo ya kipaumbele ikiwa ni pamoja na kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu kwa kuweka mkazo katika upatikanaji wa huduma bora za jamii ikiwemo elimu, maji, afya, umeme na barabara.
Ametaja maeneo mengine ni ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda kwa kuimarisha sekta ya kilimo kwa kujenga viwanda vitakavyotumia malighafi inayopatikana nchini, kuimarisha mashirika ya viwanda na kuanzisha na kuendeleza maeneo ya viwanda.
Waziri Mkuu ameyasema hayo jana (Ijumaa, Novemba 15, 2019) wakati akiahirisha mkutano wa 17 wa Bunge la 11 jijini Dodoma. Amewasisitiza wananchi kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na uzalendo ili kuiwezesha nchi kufikia malengo ya kujenga uchumi imara, unaojitegemea na wenye kuweza kuhimili ushindani.
“Ujenzi wa mazingira wezeshi katika kuendeleza miundombinu itakayosaidia maendeleo ya biashara na uwekezaji nchini; kuhakikisha Watanzania wenye sifa stahiki wanapewa kipaumbele katika kandarasi au ajira zinazotokana na utekelezaji wa miradi ya kimkakati.”
Amesema eneo lingine ni kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa Mpango. Baada ya tathmini ya utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/2017–2020/2021 kwa lengo la kuimarisha usimamizi na kuanza maandalizi ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/2022–2025/2026).
Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kusisitiza Maafisa Masuuli wazingatie maeneo ya kipaumbele yaliyoainishwa katika Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo na wahakikishe kamati za mipango na bajeti katika mafungu yao zinatekeleza majukumu yake ipasavyo. “Serikali kwa upande wake itaandaa mipango ya kisekta, kitaasisi na kimaeneo ambayo utekelezaji wake utachochea ujenzi wa uchumi wa viwanda, mageuzi ya uchumi na maendeleo ya watu.”
“Katika udhibiti wa matumizi, naendelea kuwasisitiza Maafisa Masuuli wahakikishe wanatumia mfumo wa kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (Tanzania National Electronic Procurement System – TANePS). Hivyo, kila taasisi ya nunuzi ihakikishe inatumia mfumo huo kabla ya tarehe 31 Desemba 2019.
Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa upande wake itaendelea kufanya maboresho makubwa katika sekta zinazogusa wananchi moja kwa moja na kuhakikisha kuwa matunda ya kukua kwa uchumi yanawafikia wananchi.
“Watanzania wanatakiwa kuendelea kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, katika kipindi hiki ambacho amekuwa akichukua hatua za makusudi kuhakikisha anajenga uchumi imara, kuboresha kipato na hali ya maisha ya wananchi.”
Amesema matunda ya maboresho hayo yanayoendelea yanaonekana katika maeneo mengi. “Ndani ya miaka 26 kuanzia 1991/1992 hadi 2017/2018 kiwango cha umaskini wa mahitaji ya msingi kimeweza kupungua kwa asilimia 13. Kadhalika, umaskini wa chakula nao umepungua kutoka asilimia 10 mwaka 2011/12 hadi asilimia 8.0 mwaka 2017/18.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema katika kuelekea msimu wa kilimo wa 2019/2020 hali ya upatikanaji wa chakula nchini imeendelea kuimarika kutokana na uzalishaji mzuri wa mazao ya chakula kwa msimu 2018/2019, ambao ulifikia tani milioni 16.41 ikilinganishwa na mahitaji ya tani milioni 13.84 na kuiwezesha nchi kujitosheleza kwa mahitaji ya chakula kwa asilimia 119.
Amesema pamoja na uzalishaji huo mzuri, kumekuwepo na mahitaji makubwa ya nafaka katika baadhi ya maeneo kutokana na hali ya mvua kutokuwa nzuri na kuwepo kwa dalili za kupanda bei za nafaka, Serikali imetoa maelekezo kwa Wakala wa Hifadhi ya Chakula ya Taifa kuhakikisha inasambaza nafaka kwenye maeneo yenye upungufu ili kukabiliana na changamoto ya kupanda kwa bei.
“Nitumie fursa hii kuwahimiza wakulima kutumia vizuri mvua za vuli zinazoendelea kunyesha maeneo mengi ya nchi yetu kwa kupanda mazao yanayostahimili ukame na ekolojia ya maeneo husika. Aidha, tukumbuke pia kujiwekea akiba ya kutosha ya chakula kwa ajili ya matumizi ya kaya baada ya mavuno badala ya kuuza chakula chote.”
Kuhusu upatikanaji wa pembejeo, Waziri Mkuu amesema katika kuhakikisha wakulima wanapata mbolea kwa wakati na bei nafuu, Serikali imetoa bei elekezi kwa mbolea aina ya DAP na UREA ambazo zipo katika Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja. “Hivyo, nitumie fursa hii kuzikumbusha mamlaka husika kuhakikisha kwamba bei elekezi zinafahamika kwa wakulima katika maeneo yote na wauzaji wanauza kwa kuzingatia bei hizo.”
Pia, Waziri Mkuu amezungumzia kuhusu masoko ya mazao ya kilimo ambapo amesema licha ya kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao mbalimbali nchini, kumekuwepo na changamoto kadhaa za upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa baadhi ya mazao ikiwemo la pamba, korosho na tumbaku.
Amesema changamoto hizo zinachangiwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko na mwenendo wa bei katika soko la dunia pamoja na uwezo mdogo wa kuchakata mazao hayo nchini, hivyo Serikali inaimarisha mifumo ya masoko ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, kuongeza tija na kupunguza gharama za uzalishaji kwa kuimarisha viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.
“Hatua hizi zitasaidia kuongeza thamani ya mazao na hivyo, kuimarisha bei. Kwa sasa tunaendelea na msimu wa mauzo wa zao la korosho baada ya mazao ya pamba na kahawa kumaliza. Minada ya korosho inaendelea vizuri. Viongozi wa Mikoa na Wilaya wasimamie malipo kwa wakulima na kuhakikisha wanalipwa kwa wakati.”