Hivi karibuni, Serikali ya Tanzania ilipata fedha za kutekeleza mradi wa kuzuia kuenea kwa sumukuvu hapa nchini (TANIPAC). Mradi huo unalenga kupunguza kutokea kwa madhara ya sumukuvu katika mfumo wa chakula kupitia udhibiti husishi kwenye mnyororo wa thamani wa mazao ya mahindi na karanga, hivyo kuboresha uhakika na usalama wa chakula na hatimae kuimarisha afya na lishe ya jamii yetu na kuimarisha biashara kati ya Tanzania na nchi zinazotuzunguka.
Mradi huo unatekelezwa kwa kuzingatia mkakati Madhubuti kwa kushughulikia masuala yote yanayohusu sumukuvu hapa nchini. Mkakati huo unazingatia udhibiti wa sumukuvu katika hatua za uzalishaji, uvunaji, udhibiti wa kibilojia, teknolojia baada ya kuvuna na njia za ukaushaji, uhifadhi, kujenga uwezo wa kitaasisi, uratibu na kutoa elimu ya kuhamasisha wadau muhimu. Ushiriki wa sekta binafsi ni muhimu katika uhaulishaji wa teknolojia pamoja na kuhakikisha mradi unakuwa endelevu.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 4 Novemba 2019 wakati akifungua Mkutano wa kwanza wa Afrika wa kudhibiti Sumkuvu (Alfasafe) kwenye vyakula uliofanyika katika Hoteli ya Mount Meru Jijini Arusha.
Mhe Hasunga amesema kuwa Ushirikiano wa kiutafiti, kati ya sekta binafsi na watunga sera, ni muhimu katika kufanikisha mageuzi ya kilimo.
Waziri Hasunga amesema kuwa Tangu kuibuka kwa tatizo la sumukuvu mwaka 2016, Tanzania imechukua hatua mbalimbali za kupunguza kusambaa kwa sumukuvu hapa nchini. Kwa kutambua changamoto za kukabili sumukuvu, ambapo kunahitajika kutumia njia mbalimbali kuanzia kwenye hatua za uzalishaji, uvunaji, uhifadhi, usindikaji na kuhusisha sekta za Umma na Binafsi katika kupunguza upotevu wa chakula na kuongeza upatikanaji wa chakula salama na lishe bora.
Amesema, Tanzania imeanzisha Kamati Jumuishi ya Uendeshaji inayohusisha sekta na taaluma kutoka taasisi mbalimbali chini ya Uenyekiti wa Wizara ya Kilimo ambayo ina mamlaka ya kusimamia masuala yote yanayohusu sumukuvu.
Kadhalika, amewahakikishia washiriki hao kuwa kinga ya sumukuvu - Alfasafe TZ01; imeshasajiliwa kwa matumizi hapa nchini Tanzania. "Aidha, nimefarijika kuwa kazi hii inafanywa na Kampuni Binafsi ambayo imewekeza katika uzalishaji, na usambazaji wa bidhaa hii ambayo itaokoa Maisha ya watu hapa nchini" Alisisitiza
"Napenda kuwahakikishia utayari wa Wizara yangu katika kuyatumia maazimio mtakayokubaliana katika mkutano huu. Aidha, Serikali ya Tanzania, inatilia maanani na inaunga mkono hatua zinazochukuliwa katika kuhimiza biashara ya chakula salama, usalama wa chakula na lishe" Alisema Mhe Hasunga
Tanzania kwa sasa inatekeleza Awamu ya Pili Programu ya Uendelezaji wa Sekta ya Kilimo (ASDP II) yenye lengo la kuleta mageuzi ya sekta ya kilimo kuwa na kilimo chenye tija na kibiashara, pamoja na kukuza uchumi wa wakulima wadogo na kuboresha maisha, uhakika wa chakula na lishe bora.
Uhakika wa chakula na lishe ni muhimili ambao ni muhimu wa ASDP II Katika kufikia malengo hayo, uwekezaji katika utafiti wa kilimo ni muhimu katika kuleta matokeo kwa wakulima na wadua wengine katika mnyororo wa thamani.
Waziri Hasunga amesema kuwa kutokana na takwimu za Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) za mwaka 2017, Tanzania inaongoza katika uzalishaji wa mahindi na karanga katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki, kwa kuzalisha tani milioni 6 na tani milioni moja mtawalia.
Amesema, Pamoja na mafanikio hayo, Serikali inatambua kuwa, ingawa mazao hayo ni muhimu kwa chakula cha kila siku, lakini yanakabiliwa na ukubwa wa tatizo la sumukuvu ambalo linahatarisha usalama wa chakula na kuwa kikwazo cha biashara ya mazao hayo kwa nchi jirani na Tanzania.
Mkutano huu ambao umewaweka pamoja watafiti, wafanyabiashara, watunga sera na wadau wa maendeleo, ambao unalenga kupanga mikakati ya kuongeza kasi ya matumizi ya kinga ya sumukuvu (Alfasafe), na kukabili sumukuvu barani Afrika, unadhihirisha mabadiliko chanya ya kimtazamo tunayoyahitaji.