NEWS

2 Desemba 2019

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Chashiriki Safari Ya Majaribio Ya Treni Ya Abiria Kutoka Dar Es Salaam Kwenda Moshi Kilimanjaro

Tarehe 1 Disemba 2019, Ndg. Humphrey Polepole Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ameshiriki safari ya kwanza ya majaribio ya treni ya abiria kutoka Dar Es Salaam kwenda Moshi, Kilimanjaro.

Ndg. Polepole amesema kuanza kwa safari hii ya kwanza ya majaribio kutoka Dar es Salaam kwenda Moshi, Kilimanjaro ni sehemu ya Maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015-2020 katika eneo la usafiri na usafirishaji wa watu na mizigo ambapo miradi mikubwa mitatu inatekelezwa kwa pamoja ikiwamo; ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa (standard gauge railway -SGR) kutoka Dar mpaka Makutopola, Dodoma awamu ya kwanza, maboresho makubwa ya reli ya kati kutoka Dar Es Salaam mpaka Isaka ili kuiongezea ufanisi na ubebaji mzigo mkubwa zaidi pamoja na ufufuaji na ukarabati mkubwa wa reli njia ya kaskazini inayojumuisha Mikoa ya Dar Es Salaam, Pwani, Tanga na Kilimanjaro awamu ya kwanza.

Treni hiyo ya abiria inayofanya safari yake ya kwanza ya majaribio tangu iliposimamishwa kutoa huduma hiyo miaka 25 iliyopita imevutwa na kichwa cha kisasa cha treni “9013 Classic” na imefunga mabehewa 9 yakiwamo mabehewa ya daraja la kwanza, daraja la pili, daraja la tatu, behewa lenye mgahawa unaotoa vyakula vya aina yote, vinywaji baridi na vikali pamoja na behewa la uendeshaji, usalama na usimamishaji wa treni.

Safari hii ya kwanza na ya kihistoria imeleta hamasa kubwa mno ambapo katika kila stesheni mamia ya wananchi walizuia treni kwa shangwe, nderemo na vifijo.

Ndugu Polepole amepongeza uongozi wa Shirika la Reli kwa kuipanga kwa mafanikio safari hii ya kwanza ya treni ya abiria na ametoa rai kwa vyombo vya ulinzi na usalama na Shirika kuimarisha ulinzi na kutoa elimu ya ujirani wema kati ya reli na jamii ziishizo pembezoni mwa reli ili kuitunza na kuilinda reli hii muhimu kwa maendeleo.

Pamoja na Ndg. Polepole Katibu wa itikadi na Uenezi wa CCM, watendaji wa Shirika la Reli wameongozwa na Ndg. Masanja Kadogosa, Mkurugenzi Mkuu wa TRC na Maafisa waandamizi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa usafiri wa ardhini (LATRA).

Imetolewa na,
IDARA YA ITIKADI NA UENEZI
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)