NEWS

14 Desemba 2020

Rais Magufuli atuma salamu za rambirambi kufuatia ajali ya Singida

Rais Dkt John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia za watu 14 waliofariki dunia katika ajali ya barabarani iliyotokea katika kijiji cha Mkiwa wilaya ya Ikungi mkoani Singida.

Ajali hiyo imetokea katika barabara kuu ya Singida – Dodoma ambapo basi dogo lililokuwa limebeba watu waliokuwa wametoka Mwanza kwenda Itigi wilayani Manyoni liligongana uso kwa uso na lori la mizigo lililokuwa linatoka Dar es salaam kwenda Kahama mkoani Shinyanga na kusababisha vifo hivyo pamoja na majeruhi watatu.

Rais Magufuli amemtaka mkuu wa mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi kufikisha salamu zake za pole kwa wafiwa wote, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na vifo hivyo na amesema anaungana na familia hizo katika kipindi hiki cha majonzi.

“Nawapa pole wafiwa wote, Mwenyezi Mungu awatie nguvu, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na wapendwa wenu, nawaombea Marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi na majeruhi wote wapone haraka,” amesema Rais Magufuli.

Amevitaka vyombo vyote vinavyosimamia usalama wa barabarani, kuongeza jitihada za kudhibiti ajali hasa katika kipindi hiki cha kufunga mwaka ambapo kumekuwa kukitokea ajali nyingi za barabarani, na pia amewataka watumia barabara wote kuwa makini na kujiepusha kuvunja sheria na taratibu za barabarani