NEWS

17 Desemba 2020

Wanafunzi 219 wakatiza masomo kwa kubeba ujauzito Mwaka 2020 Mkoani Simiyu


Samirah Yusuph
Bariadi.
Katika kipindi cha januari hadi novemba 2020 wanafunzi 219 kati ya hao 42 wa shule za msingi na 177 wa shule za sekondari wamekatiza masomo kwa kupata ujauzito wakiwa shuleni.

Hali hiyo imetajwa kuwa ni tatizo kubwa kwa shule za sekondari hasa katika wilaya ya Busega na Maswa ambazo zimekuwa na idadi kubwa ya wanafunzi hao kwa shule za msingi na sekondari.

Katika mwaka 2019 Busega kulikuwa na wanafunzi  waliopata mimba 64 sekondari 59 na msingi 5, Maswa 72 sakondari 57 na msingi 15, Bariadi Mji 12 sekondari 10 msingi 2, Meatu 18 sekondari 11 na msingi 7, Bariadi vijijini 14 sekondari 11 na msingi 3 na itilima 14 sekondari zikiwa mimba 5 na msingi mimba 2.

Kwa mwaka 2020 wilaya ya Busega wanafunzi waliopata mimba ni 89 msingi wakiwa 14 na sekondari 75, Maswa 68 msingi 11 na sekondari 57, Bariadi vijijini 22 sekondari 15 na msingi 7 huku sababu kubwa ya ongezeko hilo likitajwa kuwa ni kuibua kesi za mimba katika jamii.

Akifafanua kesi hizo mratibu wa Afya shuleni mkoa wa Simiyu Jusline Bandiko alisema kuwa kufufua kesi hizo imepelekea kugudua idadi kubwa ya wanafunzi wanaokatiza masomo kwa sababu ya mimba tofauti na hapo awali ambapo wazazi walimaliza tatizo hilo kienyeji kwa kulipana faini.

"kwa sasa wanawafuatilia wanafunzi kwa ukaribu ili kuweza kubaini sababu ambazo zinapelekea kukatiza masomo hivyo inakuwa ni rahisi kugundua kesi za mimba lakini pia tunaendelea kutoa elimu lika kwa wanafunzi ili waweze kutambua afya ya uzazi pamoja na kuepuka mimba hizo",Alisema Jusline.

Kwa upande wao baadhi ya wazazi wa wilaya ya Busega na Bariadi walieleza kuwa uwepo wa shughuli za uvuvi na uchimbaji wa madini imekuwa ni kichocheo cha watoto wengi kubeba ujauzito kutokana na uangalizi mdogo wa wazazi.

"Hizi mimba zinachangiwa na malenzi hususani katika maeneo yetu haya ya machimbo, watoto wanakuwa wanajilea wanaona namna ambavyo wadada wanavyojiuza na wao wanaiga ndio sababu wanaambulia ujauzito;"alisema Maria Zakaria mkazi wa kijiji cha Lubaga Dutwa.
 
Aidha Hadi sasa tayari uongozi wa mkoa mkoa umeunda kamati maalum ambayo itahuaisha watoa elimu lika pamoja na vyombo vya usalama ili kuhakikisha wanakomesha tatizo la mimba kwa kutoa elimu ya kujitambua kwa wanafunzi pamoja na wazazi.
 
Mwisho.