NEWS

22 Januari 2021

Balozi Ibuge akutana, kufanya Mazungumzo na Mwanansheria Mkuu wa Zanzibar


Na Nelson Kessy, Zanzibar
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amekutana na kufanya mazungumzo na Mwanansheria Mkuu wa Zanzibar Dkt. Mwinyi Talib Haji katika Afisi za Mwanasheria Mkuu mjini Zanzibar

Mazungumzo hayo yamelenga kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu ya kazi baina Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Balozi Ibuge amesema kuwa jukumu kubwa la watendaji wa Serikali hizi mbili ni kuhakikisha wanatekeleza maono (vision) viongozi wakuu wa Serikali hasa kwa kuzingatia maelekezo yaliyopo katika ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). “Ni jukumu letu sisi kama watendaji wa serikali kuwasaidia viongozi wetu kutekeleza maoni ya viongozi wetu kwa kuzingatia Ilani ya CCM ya 2020 – 2025,” Amesema Balozi Ibuge.

Kwa upande wake Dkt. Mwinyi Talib Haji amemuahidi Balozi Ibuge kuwa wataendelea kushirikiana katika kuhakikisha kuwa malengo ya serikali zote mbili yanatekelezwa kwa maslahi mapana ya pande zote mbili. “Nakuahidi kuwa sisi kama Afisi ya Mwanasheria Mkuu – Zanzibar tutashirikina na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikino wa Afrika Mashariki katika kuhakikisha tunatekeleza majukumu ya serikali,” Amesema Dkt. Haji.