NEWS

10 Januari 2021

Makampuni Yasiyokamilisha Urasimishaji Yanyang’anywe Kazi -Naibu Waziri Mabula


 Na Munir Shemweta, WANMM ARUSHA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameagiza Makampuni ya Urasimishaji ambayo mikataba yake imekwisha na kushindwa kukamilisha kazi kwa wakati katika mkoa wa Arusha yanyang’anywe kazi hizo na kurejesha fedha zilizotolewa na wananchi sambamba na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Aidha, alielekeza kuwa kwa yale  makampuni ambayo muda wa kazi bado haukuisha basi yafanye kazi chini ya uangalizi ili kuhakikisha kazi waliyopewa inakamilika kwa wakati.

Dkt Mabula alitoa agizo hilo tarehe 9 Januari 2021 katika mkoa wa Arusha alipozungumza na watendaji wa sekta ya ardhi na wakurugenzi wa halmashauri akiwa katika ziara yake ya siku moja kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kuhamasisha ukusanyaji kodi ya pango la ardhi.

Naibu Waziri wa Ardhi aliongeza kwa kusema kuwa, kufuatia uamuzi huo Makatibu Tawala wa Wilaya katika mkoa wa Arusha watumie mamlaka zao kuunda vikosi kazi kushirikisha halmashauri ili kuharakisha zoezi la urasimishaji kwenye maeneo ambayo makampuni ya urasimishaji yameshindwa kukamilisha kazi.

Awali Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Mabula akizungumza na Makampuni ya urasimishaji alisema, baadhi yake yameshindwa kukamilisha kazi kwa wakati kwa visingizio mbalimbali na hata pale yalipokutana na Waziri wa Ardhi William Lukuvi Dar es Salaam na kuongezewa muda kukamilisha kazi  yalishindwa na kusababisha malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya zoezi hilo.

“Makampuni ambayo mikataba yake iimekwisha na kufikia Januari 31, 2021 hayajakamilisha kazi, basi yafungashe virago na kupelekwa katika vyombo vya sheria na halmashauri zishirikiane na ofisi za ardhi za mkoa kufanya kazi hiyo” alisema Dkt Mabula.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Ardhi  Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameshangazwa na halmashauri kuweka malengo madogo katika ukusanyaji maduhuli ya Serikali yatokanayo na kodi ya  ardhi bila kujumuisha madeni ya wadaiwa sugu.

Alisema, mkoa wa Arusha wenye wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi zaidi ya 200 una madeni ya zaidi ya bilioni 178.943 lakini mkoa ulijiwekea malengo ya kukusanya bilioni 8.9 tu na kufanikiwa kukusanya bilioni 4.2 sawa na asilimia 47 kufikia desemba 2020.

Aliwaelekeza Maafisa Ardhi Wateule kuhakikisha inawafikisha kwenye Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya wadaiwa wote sugu wa kodi ya pango la ardhi kwa kuwa tayari walishapelekewa ilani za madai kama sheria inavyoelekeza na kusisitiza kuwa, kwa wale wadaiwa wanaotaka majadiliano yafanyike ndani ya siku kumi na nne na baada ya hapo shauri lipelekwe kwenye  Baraza.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, serikali inahitaji mapato kwa ajili ya kuendesha miradi mbalimbali ya kimaendeleo na kusisitiza kuwa huko katika Mabaraza ya Ardhi maamuzi yake ni kulipa ama kunadiwa mali kufidia deni.

Baadhi ya Wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi zikiwemo taasisi mbalimbali katika jiji la Arusha kama vile Chuo cha Uhasibu na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) walikubali kulipa madeni yao kwa awamu ambapo Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Mabula alielekeza kuingia makubaliano kwa maandishi.

Halmashauri ya jiji la Arusha pekee inadai jumla ya shilingi bilioni 4,134,610,533.23 za wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi na jiji hilo  limeweza kukusanya bilioni 2.27 sawa na asilimia 49.79 ya lengo kwa mwaka 2020/2021 ambalo ni bilioni 4.134.